Jamii FM
Jamii FM
16 June 2025, 17:17 pm

Wakulima wa mazao ya ufuta na korosho wa kijiji cha Imekuwa wamekuwa wakipambana uanzishwaji wa chama cha ushirika tangu mwaka 2023 bila mafanikio kwa kile kinachoelezwa kutokidhi vigezo vya unazishaji wake
Na Musa Mtepa
Baadhi ya wakulima wa mazao ya korosho na ufuta kutoka Kijiji cha Imekuwa, Kata ya Naumbu, Halmashauri ya Mtwara vijijini, wamelazimika kuuza mazao yao kupitia Chama cha Jirani cha msingi cha ushirika Ndumbwe.
Hatua hiyo inatokana na kutoridhishwa kwao na utendaji wa Chama cha Msingi cha Mayanga, ambacho kimekuwa kikihudumia wakulima hao kwa muda mrefu.
Wakizungumza na Jamii FM Radio, wakulima hao wamesema kuwa wameamua kupambana kuhakikisha wanapata chama chao cha ushirika kitakachokuwa na uwezo wa kushughulikia changamoto zinazowakabili kwa sasa.
Hata hivyo, licha ya juhudi hizo, wakulima wamesema wamekuwa wakikumbana na changamoto mbalimbali zinazowarudisha nyuma katika mchakato wa kuanzisha chama chao kipya.
Akielezea hatua walizozichukua kuhakikisha wanapata chama chao, Bw. Yusufu Hassani, mkazi wa Kijiji cha Imekuwa na mfuatiliaji wa karibu wa mchakato huo, amesema tayari waliwasilisha taarifa rasmi kwa mkurugenzi wa halmashauri, wakieleza kuwa idadi ya wakulima na kiwango cha uzalishaji kilichopo kinatosha kuanzisha chama kipya cha ushirika.
Kwa upande wake, Bw. Hamisi Ausi, meneja wa Mayanga AMCOS, amesema chama hicho hakijashindwa kuwahudumia wanachama wake na kwamba utaratibu wa kawaida unaendelea. Ameeleza kuwa baadhi ya wakulima wanaotajwa kuhama chama si wanachama wa Mayanga kwa mujibu wa kumbukumbu zao.
Kuhusu tuhuma za viongozi wa Mayanga AMCOS kuhusika katika kuwazuia wakulima kuanzisha chama chao, Bw. Ausi amekanusha madai hayo, akibainisha kuwa jukumu la kusajili chama kipya ni la Afisa Ushirika pamoja na Msajili wa Vyama vya Ushirika ngazi ya mkoa, kwa kuzingatia taratibu zilizowekwa.
Akizungumza katika kikao cha utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mrajisi msaidizi wa vyama vya ushirika mkoa wa Mtwara, Bi. Grace Masambaji, amesema kutokana na ongezeko la vyama vya ushirika pamoja na utendaji usioridhisha, ofisi yake haitasajili vyama vipya kwa sasa, badala yake italenga kupunguza idadi ya vyama hivyo ili kuboresha utendaji wake.
