Jamii FM

INEC yafanya mkutano na wadau wa uchaguzi Mkoani Mtwara

16 January 2025, 13:40 pm

Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Mhe. Jaji Jacob Mwambegele akizungumza na wadau wa uchaguzi leo january 16,2025 katika ukumbi wa BOT Mtwara(Picha na Mtwara RS habari)

Huu ni mkutano uliohusu mada kuu ya maandalizi ya uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura kwa wadau katika mkoa wa Mtwara uliohusisha viongozi wa vyama vya siasa, asasi za kiraia, makundi maalum, kamati za ulinzi na usalama, wahariri na waandishi wa habari mkoani Mtwara.

Na Musa Mtepa

Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imefanya mkutano na wadau wa uchaguzi kuhusu uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura mkoani Mtwara. Mkutano huu ulifanyika leo, Januari 16, 2025, kwenye ukumbi wa mikutano wa Benki Kuu ya Tanzania (BOT) tawi la Mtwara.

Akizungumza katika mkutano huo, Mwenyekiti wa Tume huru ya Taifa ya uchaguzi, Mhe. Jaji Jacob Mwambegele, amewaasa wananchi kujiepusha na kosa la kujiandikisha zaidi ya mara moja ili kuepuka uvunjaji wa sheria.

Jaji Mwambegele amewakumbusha viongozi wa vyama vya siasa na wadau wa uchaguzi kuzingatia sheria ya uchaguzi, kanuni za uboreshaji, na maelekezo ya tume pamoja na kusimamia miiko na mipaka ya uendeshaji wa zoezi la uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.

Sauti ya 1: Jaji Jacob Mwambegele (Mwenyekiti wa INEC)


Aidha, Jaji Mwambegele amesisitiza umuhimu wa viongozi wa vyama vya siasa na wadau wa uchaguzi kusimamia na kuhamasisha wananchi kujiandikisha kwa ufanisi katika zoezi la uboreshaji.

Sauti ya 2: Jaji Jacob Mwambegele (Mwenyekiti wa INEC)

Kwa upande wa wawakilishi wa asasi za kiraia mkoani Mtwara, Komba Baltazar kutoka FAWOPA na Bi. Mariamu Chimbwahi kutoka KIMWAM wameelezea furaha yao kwa kushirikishwa katika mkutano huku wakiahidi kuwa mabalozi kutoa elimu kwa wananchi kuhusu uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.

 Sauti ya Komba Baltazar na Mariamu Chimbwahi (Wawakilishi wa Asasi za Kiraia)

Ismail Liuye, kiongozi wa chama cha NCCR-MAGEUZI mkoa wa Mtwara, amesema kuwa viongozi wa vyama vya siasa wameridhishwa na maelekezo yaliyotolewa na tume, na kuahidi kuwa wao kama viongozi watahamasisha wananchi na viongozi wa chini kwenda kujiandiksha.

Sauti ya Ismail Liuye (Kiongozi wa NCCR-MAGEUZI)

Mkurugenzi wa MERODI, Frances Chiwango, amezungumzia changamoto wanazokutana nazo watu wenye ulemavu, akieleza kuwa kuna changamoto za miundombinu za kufikia maeneo ya uandikishaji, na mkanganyiko wa majina kwa watu wenye ulemavu wa kusikia.

Sauti ya  Frances Chiwango (Mkurugenzi wa MERODI)

Viongozi wa dini mkoani Mtwara wameshukuru tume huru ya taifa ya uchaguzi kwa kuwashirikisha katika mkutano huu na kuwataka vijana na wananchi kuwa makini katika maandalizi ya uchaguzi ujao.

Sauti ya Viongozi wa Dini Mtwara
Washiriki wa mkutano wa tume huru ya taifa ya uchaguzi wakishiriki mkutano huo

Kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022, jumla ya wapiga kura 5,586,433 wanatarajiwa kuandikishwa katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura, ikiwa ni asilimia 18.7 ya wapiga kura 29,754,699 waliopo kwenye Daftari baada ya uboreshaji wa 2019/2020. Ambapo Kwa mkoa wa Mtwara, tume inatarajia kuandikisha wapiga kura 174,719, ikiwa ni ongezeko la asilimia 18.7 ya wapiga kura 930,840 waliopo kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura

Zoezi la uboreshaji linaendelea na linatarajiwa kuwa na mchango mkubwa katika kuhakikisha uchaguzi ujao unafanyika kwa usawa na uwazi.