Jamii FM

Mkoa wa Mtwara waomba Baraza la mitihani kukanusha Matokeo mtandaoni

16 January 2021, 13:15 pm

Mkuu wa mkoa wa Mtwara Mh. Gelasius Byakanwa amesema taarifa zinazosambaa kwenye mitandao ya kijamii zikionyesha kwamba shule 10 za mwisho kitaifa za kidato cha nne tisa ni kutoka mkoa wa Mtwara sio za kweli na kwamba hazihusiani na matokeo halisi ya mkoa Mtwara.
 
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake leo amesema  taarifa zilizotolewa na baraza la mitihani yenye kurasa 21 hakuna kipengele kilichoandika shule 10 za mwisho kitaifa kama ilivyosambazwa kwenye mitandao ya kijamii.
 
Mh. Byakanwa ameongeza kuwa taarifa hizo zinazosambaa kwenye mitandao kuwa sio za kweli na sio sehemu ya taarifa iliyotolew na Baraza la Mitihani Tanzania (NECTA), hivyo amewataka wananchi kupuuzia uvumi huo unaosambazwa na watu wasioutakia mema mkoa wa Mtwara.
 
Baraza la Mitihani Tanzania (NECTA) jana limetangaza matokeo ya mitihani ya kujipima ya darasa la nne na kidato Cha pili na matokeo ya kidato cha nne ambapo ufaulu umepanda ukilinganisha na matokeo ya Mwaka jana.
 
Watahiniwa waliojiandikisha kufanya mtihani walikua 434,654 na waliofanya mtihani ni 373,958 huku ufaulu ukiongezeka kwa 5.19%, wasichana waliofaulu ni 193,672 sawa na 85.44% ya wasichana waliofanya mtihani na wavulana waliofaulu ni 180,286 sawa na 86.27% ya wavulana walifanya mtihani. 

Mkuu wa mkoa wa Mtwara Mh. Gelasius Byakanwa