Jamii FM
Jamii FM
13 February 2026, 08:59 am

Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Korosho Tanzania, Frances Alfred, amewataka wakulima kuzingatia upogoleaji na utibuliaji wa mashamba kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi. Amesema ruzuku za pembejeo zimeongeza uzalishaji, huku akisisitiza umuhimu wa kudumisha ubora wa korosho ili kupata bei nzuri sokoni
Na Musa Mtepa
Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Korosho Tanzania (CBT), Frances Alfred, amewataka wakulima kuendelea na zoezi la upogoleaji wa matawi ya mikorosho pamoja na utibuliaji wa mashamba yao ili kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi yanayosababisha upungufu wa maji katika mikorosho.
Ameyasema hayo Februari 11, 2026, alipokuwa akizungumza katika kipindi cha Dira ya Asubuhi kinachorushwa na Jamii FM Radio, kilichopo Naliendele, Manispaa ya Mtwara Mikindani mkoani Mtwara. Amesema kuwa katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita, moja ya changamoto kubwa iliyoikabili zao la korosho ni mabadiliko ya tabianchi, yakiwemo mvua zisizotabirika na hali ya baridi isiyotarajiwa.
Aidha, amesema mmea wa mkorosho unahitaji maji ya kutosha ili uweze kufyonza virutubisho kutoka kwenye udongo kwa ufanisi. Kutokana na taarifa za Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) zinazoonesha uwepo wa mvua za chini ya wastani, amewasisitiza wakulima kupogoa na kutibua mashamba yao ili kukabiliana na changamoto hiyo.

Hata hivyo, amesema pamoja na changamoto za mabadiliko ya tabianchi, uwepo wa pembejeo za ruzuku zinazotolewa na Serikali umechangia kwa kiasi kikubwa ongezeko la uzalishaji wa zao hilo. Ameeleza kuwa uzalishaji umeongezeka kutoka tani 300,010 mwaka 2023/2024 hadi tani 528,000 mwaka 2024/2025, hatua inayochangiwa na ruzuku hizo.

Katika hatua nyingine, amewataka wakulima wanaokabiliwa na bei ndogo kuendelea kusimamia ubora wa zao la korosho kuanzia ngazi ya vyama vya msingi hadi kwa mkulima mmoja mmoja, ili waweze kupata bei nzuri na kuongeza manufaa yatokanayo na zao hilo.
