Jamii FM
Wakulima wa Mihogo waipongeza TARI Naliendele
12 May 2023, 14:24 pm
Na Mussa Mtepa.
Wakulima wa zao la mihogo kutoka kijiji cha Mkunwa Halmashauri ya Wilaya Mtwara Mkoani Mtwara wameshukuru kituo cha utafiti na kilimo cha TARI Naliendele kwa kitendo cha kuwashirikisha kwenye utafiti wa zao hilo kwani wameweza kutambua umuhimu wa kutumia mbegu Bora na zenye tija .
Wakizungumza hayo siku ya Jana Mei 11 ,2023 wakulima hao wamesema kuwa kupitia utafiti huo wameweza kutambua mbegu Bora na zisizo na ubora hivyo zitawasaidia katika kuzitumia huku wakiomba TARI kuendelea kushirikisha wakulima katika tafiti mbalimbali ili kuwaondoa wakulima katika matumizi makubwa ya gharama za uandaaji wa mashamba na kipato duni kinachopatikana.
Mtafiti Festo Masisila kutoka TARI Naliendele akielekeza matokeo ya mbegu zilizofanyiwa utafiti mbele ya wakulima wa kijiji cha Mkunwa. (Picha na Mussa Mtepa)
Dadi Ali Likung’u mkulima kutoka kjiji cha Mkunwa amesema kitendo cha TARI Naliendele kuwashirikisha katika utafiti huo umewasaidia kujua na kutambua mbegu Bora na faida inayoweza kupatikana huku akiwashauri wakulima wengine kuendelea kutumia kituo hicho kwa mbegu zilizofanyiwa utafaiti.
Nae afisa kilimo kutoka kata ya mkunwa Musa Liponda ameipongeza TARI Naliendele kwa kitendo cha kuwashirikisha wakulima kwenye utafiti huku akiwaomba wakulima kufuatilia yale yote Bora waliyaona kwenye utafiti huo ili kulima kilimo chenye tija.
Mihogo iliyofanyiwa utafiti na Taasisi ya utafiti wa kilimo TARI Naliendele kwa kushirikiana na kijiji cha Mkunwa Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara (picha na Mussa Mtepa)
Aidha Musa Liponda amewataka wakulima wa kata hiyo kutumia mbegu zilizofanyiwa utafiti na kituo cha TARI kwa kushirikiana na maafisa kilimo wa vijiji na kata kupata mbegu hizo ili kubadilika na kuingia kwenye uzalishaji wenye tija na kuachana na kilimo cha kutumia nguvu kubwa kwa kupanda mbegu zisizo na tija.
Kwa upande wake Festo Masisila mtafiti wa mazao jamii ya mihogo na viazi kutoka kituo cha utafiti na kilimo TARI Naliendele amesema kuwa katika utafiti huo ulihusisha aina tisa(9) ya mbegu za Mihogo kwa kuwashirikisha wakulima ili waweze kutambua hizo mbegu na kuwa na machaguo ni aina ipi wanaweza kutumia katika kilimo chao.
Pia Festo Masisila amesema kuwa mbegu hizo zimethibitishwa na kuithinishwa na taasisi ya uthibiti wa Mbegu tosic Mwaka 2019 huku uzalishaji wake ukianza mwaka 2021 na mwaka 2022 zilianza kusambazwa kwa wakulima.
Akielezea dhamira ya utafiti wa kuwashirikisha wakulima amesema kuwa kutaka kuwaonesha ni jinsi gani mbegu hizo mpya zinavyozalisha na katika kuvumilia magonjwa ya mihogo ikiwemo kama vile Michirizi ya kikahawiya na Batobato kali .