Mkopo Milioni 162.7 wapamba siku ya Wanawake
9 March 2021, 09:19 am
Wananchi kata ya Nanguruwe wameonesha furaha baada ya kushuhudia baadhi ya vikundi vya wajasiriamali wakipokea mkopo wenye thamani ya Tzs. 162,770,000/= kutoka sehemu ya 10% ya mapato ya ndani ya halmashauri ya Wilaya ya Mtwara unaolenga kuwainua kiuchumi kupitia makundi ya akina Mama, Vijana na Walemavu.
Wakiongea kwa nyakati tofauti wanakikundi hao wamesema kuwa wanaishukuru sana serikali kwa utaratibu waliouweka kuwawezesha mitaji ya kuendesha biashara zao jambo ambalo limewarahisishia kupata masoko kutokana na elimu ya mara kwa mara wanayopata kabla na baada ya mkopo, Pamoja na ufuatiliaji wa karibu unaowafanya wachakalike mda wote ili kufanya marejesho.
“tukiwezeshwa tunaweza kabisa…kwahiyo tunaishukuru jumuiya ya serikali kuu na hata kutuona walemavu tukiwa na misimamo ya kufanya shughuli zetu kisha kutuunga mkono..mfano mimi napata wateja wangu wa samaki hadi Nachingwea” Nurudin Joba mwakilishi wa kikundi cha walemavu.
Aidha tukio hilo limeambatana na maadhimisho ya siku ya wananwake duniani ambapo mwaka huu imepambwa kwa kauli mbiu isemayo “Wanawake katika uongozi chachu kufikia katika Dunia yenye Usawa” ambapo mgeni rasmi alikuwa Mkuu wa Wilaya Dunstan Kyobya ambaye ameagiza wataalamu kuendelea kutoa elimu ya vikundi hasa vya akina mama.
Kwa upande wa Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya Mtwara, Bi. Erica E. Yegella ametanabaisha kuwa kiasi cha fedha kilichotolewa ni kwa robo hii ya pili ambapo ikifika robo ijayo utatolaewa mkopo mwingine kwa vikundi vitakavyokidhi vigezo, ameendelea kusema kuwa jumla ya vikundi 46 vimenufaika na mkopo huo kwa robo hii vikiwemo vinne kutoka kata ya Nanguruwe.