Mtu mmoja afariki na wengine 11 majeruhi kwenye ajali kiwandani Dangote
8 July 2021, 16:17 pm
Na Gregory Millanzi,
MTU mmoja amefariki Dunia, watatu hali zao siyo nzuri na wengine nane kujeruhiwa kufuatia ajali iliyookea kwenye Kiwanda cha kuzalisha Saruji (DANGOTE ) kilichopo Kijiji cha Hiyari halmashauri ya Wilaya ya Mtwara.
Tukio hilo limetokea Julai 7 mwaka huu majira ya saa 9:30 Alasiri ambapo udongo uliopo kwenye kinu cha kuzalisha Saruji kudondoka na kusababisha vumbi hali iliyopelekea watu hao kupata taharuki na kati yao mtu mmoja kuvua mkanda na kudondoka chini kisha kufariki wengine kupata majeraha ya moto yanayotokana na sehemu ya kinu.
Akitoa taarifa kuhusu kutokea kwa tukio hilo kwa Mkuu wa Wilaya ya Mtwara Dunstan Kyobya aliyeongozana na waandishi wa Habari, Meneja uzalishaji wa kiwandani hapo Subash Samantaray amesema kuwa Julai 5 mwaka huu walisimamisha shughuli za uzalishaji majira ya saa 12 jioni kwa ajili ya kufanya ukarabati katika kinu hicho ili kuondoa udongo ambao umeganda ndani ya kinu kinachotumika kutengeneza Saruji kiwandani hapo.
“Tulianza kuondoa maudongo udongo yale yalioganda ganda kwenye kinu husika ambacho kinatumika kutengeneza joto kwa ajili ya kutengeneza Saruji kwa muda kama wa siku tatu hivi kwahiyo wakati mchakato unataka kuanza tulitoa taarifa katika maeneo yote yale ambayo nguvu kazi itakuwa ikifanyika kwahiyo wale watu waliokuwa wakifanya Kazi kwenye lile bomba la linalopitisha mvuke kutoka kwenye chanzo kabisa cha kutengeneza joto kulitokea tukio la kudondoka dongo kubwa sana ambalo lilikuwa limeganda na kushuka chini na kutengeneza vumbi vumbi fulani likaanza kutawanyika kuelekea kwenye lile eneo ambalo watu walikuwa wamekaa”,
“Baada ya lile vumbi watu wakawa wanakimbia sasa mtu moja akafungua ule mkanda akadondoka kwahiyo jumla kulikuwa na watu 12 ambao walikuwa wanafanya kazi kwenye lile eneo walikuja kuunguzwa na huo mvuke ulivyokuwa kwenye hilo vumbi vumbi baada kudondoka huo udongo wakapata hapa huduma ya kwanza badae wakapelekwa Ligula Hospitali ya Rufaa kwa ajili ya matibabu kwahiyo yule mmoja ambaye alifungua mkanda alifariki baada ya kudondoka chini aliumia sehemu ya kichwa na wale wengine ambao walijeruhuwa wanaendelea vizuri”,amesema Samantaray