Jamii FM
Jamii FM
08/03/2026, 08:52

Kupitia maadhimisho ya siku ya wanawake Duniani (IWD), jamii inapata fursa ya kutafakari mchango, changamoto na mafanikio ya wanawake. Kwa mwaka huu, maadhimisho yamebeba kauli mbiu “Haki na Usawa kwa Wanawake na Wasichana: Msingi Jumuishi Kufikia Dira 2050.”
Gregory Millanzi na Mwanahamis Chikambu.
Katika mwanzo wa historia ya mwanadamu, kabla ya ustaarabu kujengeka na kabla jamii haijaweka mifumo ya maisha tunayoijua leo, kulikuwepo mwanamke. Mwanamke ndiye aliyebeba tumaini la uhai, mlezi wa kizazi na nguzo ya familia. Kupitia mikono yake jamii imekua, kupitia hekima yake maadili yamefundishwa, na kupitia uvumilivu wake maisha yameendelea. Tangu zamani, uwepo wa mwanamke umeendelea kuwa msingi muhimu katika kujenga na kuendeleza maisha ya binadamu.
Katika kila zama, mwanamke amekuwa kama mwanga unaoangaza njia ya maisha ya binadamu. Akiwa mama, mlezi, mwalimu na wakati mwingine kiongozi wa kimya kimya ndani ya jamii, mchango wake umeendelea kuandika sura muhimu katika historia ya maendeleo ya dunia. Ni nguvu ambayo mara nyingi haionekani wazi kwa macho, lakini athari yake imekuwa kubwa katika kujenga kizazi, kuimarisha familia na kusimika misingi imara ya jamii.

Hata hivyo, kwa miaka mingi wanawake na wasichana wamekumbana na changamoto na vikwazo mbalimbali katika nyanja tofauti za maisha. Baadhi walinyimwa fursa sawa za kupata elimu, wengine hawakupewa nafasi katika uongozi, na wengi hawakushirikishwa kikamilifu katika maamuzi muhimu yanayoathiri maisha ya jamii. Hali hii ilisababisha sauti ya mwanamke kutosikika ipasavyo licha ya mchango mkubwa aliokuwa akiutoa kila siku katika maendeleo ya familia na taifa.
Licha ya changamoto hizo, dunia inaendelea kubadilika. Leo hii, sauti ya mwanamke inazidi kusikika na nafasi yake katika jamii inaendelea kutambuliwa. Kupitia maadhimisho ya siku ya wanawake Duniani (IWD), jamii inapata fursa ya kutafakari mchango, changamoto na mafanikio ya wanawake. Kwa mwaka huu, maadhimisho yamebeba kauli mbiu “Haki na Usawa kwa Wanawake na Wasichana: Msingi Jumuishi Kufikia Dira 2050.” Makala haya yameandaliwa na Gregory Millanzi akishirikiana na Mwanahamis Chikambu.