Uzinduzi wa Mwenge na mafanikio ya kupambana na UKIMWI
1 April 2023, 23:07 pm
Na Mussa Mtepa
Waziri Mkuu wa Tanzania Mh. Kasim Majaliwa amewataka wakimbiza mwenge kitaifa kukagua na kujiridhisha na ubora wa Miradi ya Maendeleo itakayokaguliwa ili ilingane na thamani ya fedha zilizotolewa kwenye mradi husika na kuahidi kuzifanyia kazi taarifa zote za Rushwa na ubadhirifu utakaobainika kufanywa katika mradi husika.
Vifo vinavyotokana na UKIMWI vimeshuka kutoka 65,000 mwaka 2010 hadi 29,000 kwa mwaka 2021
Akizungumza kwenye Uzinduzi wa Mbio za Mwenge kitaifa zilizozinduliwa leo April 1, 2023 katika viwanja vya Nangwanda Sijaona Mkoani Mtwara, Waziri Mkuu amesema vitendo vya Rushwa na ubadhilifu vinadumaza upatikanaji wa Maendeleo na huduma za jamii hivyo wakimbiza Mwenge hawana budi kumulika miradi ya maendeleo na kujiridhisha ubora wake kulingana na fedha zilizoletwa juu ya mradi husika.
Aidha Waziri Mkuu Kasimu Majaliwa amesema kuwa kutokana na Jitihada za serikali na kushirikana na Wadau mbalimbali Tanzania imepiga hatua mzuri ya kufikia malengo ya kidunia ya 95.3% ya maambukizi ya virusi vya UKIMWI ifikapo mwisho wa mwaka 2025 huku kwasasa wastani wa maambukizi Mapya yamepungua kutoka wastani wa Laki moja na Kumi kwa mwaka 2010 hadi kufikia 54,000 kwa mwaka 2021, huku vifo vinavyotokana na UKIMWI vikiwa vimeshuka kutoka 65,000 mwaka 2010 hadi 29,000 kwa mwaka 2021.
“Tunza Mazingira, Okoa vyanzo vya maji kwa ustawi wa viumbe hai na uchumi wa Taifa’’
Sambamba na hilo amesema kushuka kwa idadi ya vifo imetokana na kuimarika na kusambaa kwa huduma ya matibabu na matumizi ya ARV nchini pamoja na Elimu ya kujikinga na maambukizi Virusi vya UKIMWI kuimarika.
Mbio za Mwenge wa uhuru kwa mwaka 2023 zinatarajia kukimbizwa katika mikoa 31, Halmashauri 195 huku kauli mbiu za mwaka huu ikiwa ‘’Tunza Mazingira, Okoa vyanzo vya maji kwa ustawi wa viumbe hai na uchumi wa Taifa’’.