Mpanda FM

Wananchi Konamnyagala Wapongeza Jitihada za Kamati ya Shule

7 April 2023, 7:04 am

KATAVI

Wananchi wa Kona ya Mnyagala Kijiji cha Ikaka kata ya Mnyagala Halmashauri ya Tanganyika mkoani katavi wamepongeza Jitihada za Kamati ya Shule katika usimamiaji wa upatikanaji wa Chakula shuleni hapo.

Wakizungumza na kituo hiki wamesema kuwa wameitikia Wito wa Uchangiaji wa Chakula kwa ajili ya Watoto wao wanaosoma katika shule ya msingi konamnyagala.

Balozi wa Kona mnyagala Rajabu Athumani amesema kuwa zoezi la uchangiaji wa Chakula shuleni ni endelevu na linasaidia kwa wanafunzi kuwa na usikivu darasani.

Akizungumzia suala hilo Makamu mwenyekiti wa Kamati ya shule ya msingi konamnyagala amesema kuwa wamekusanya Gunia 6 za Mahindi yaliyokobolewa na Maharage Debe 2 kwa sasa na kutoa wito kwa wananchi na wazazi wanaosomesha watoto katika shule hiyo kuendelea kujitolea katika mchango wa chakula.

Shule ya msingi konamnyagala iliyopo kijiji cha Ikaka kata ya Mnyagala Halmashauri ya Tanganyika imeanzishwa kwa nguvu za Wananchi ikiwa na Vyumba 6 vyenye wanafunzi 541.