Mtwara ipo salama dhidi ya Kimbunga “Jobo”
24 April 2021, 16:07 pm
Na Karim Faida
Mamlaka ya hali ya hewa Tanzania TMA imetangaza uwepo wa kimbunga jobo katika bahari ya Hindi, Baada ya kupokea taarifa hiyo kumekuwa na watu wanaosambaza taarifa kwenye mitandao kwamba kimbunga hicho tayari kimeshafika katika mkoa wa Mtwara.
Akiongea na waandishi wa habari leo ofisini kwake, Mkuu wa wilaya ya Mtwara Ndugu Dunstan Kyobya amesema Mtwara ipo salama tofauti na kile kinachoendelea kwenye mitandao na amewatoa hofu wanamtwara juu ya uvumi huo.
“Nisikitike kwamba kuna watu wanasambaza uvumi kuwa kimbunga jobo kimeshafika Mtwara wakati si kweli, Nimeongea na mkuu wa wilaya ya Masasi, Nanyumbu, Tandahimba na Newala hali katika wilaya zote ipo sawa” Amesema Ndugu Kyobya.
Hata hivyo ametoa onyo kwa wale wote waliohusika na kutengeneza na kusambaza taarifa hiyo kwamba wakibainika sheria itachukua mkondo wake kwa mujibu wa sheria za Tanzania.
Nae Meneja wa hali ya hewa kanda ya kusini ndugu Daudi Amasi amesema upepo na manyunyu ya mvua yaliyopo Mtwara kwa sasa ni ya kawaida. Akisoma taarifa ya Mamlaka ya hali ya hewa Tanzani, Ndugu Amasi amesema,”Kimbunga Jobo kipo umbali wa km 200 mashriki mwa Kisiwa cha Mafya, kimbunga hicho kimepungua nguvu baada ya kuingia katika mazingira yenye mzunguko wa upepo kinzani, Jobo kwa sasa ni kimbunga hafifu”