Mtwara na matarajio lukuki kisima cha maji kinachodhaniwa kuwa na gesi
21 October 2024, 18:41 pm
Kuwepo kwa dhana ya gesi katika eneo la kuchotea maji katika kijiji cha Mnyundo wananchi wamekuwa na matarajio ya makubwa ya kuona wanabadilika kimaendeleo ikiwepo kujengewa miradi ya maendeleo kama vile maji na uimarishaji wa huduma za afya.
Na Musa Mtepa
Wananchi wa Kijiji cha Mnyundo, kata ya Ndumbwe, halmashauri ya Mtwara vijijini, wana matumaini makubwa ya maendeleo kutokana na uwepo wa kisima cha maji kinachodhaniwa kuwa na gesi asilia.
Katika mahojiano na Jamii FM Redio leo, tarehe 21 Oktoba 2024, wananchi wamesema wanatarajia kubadilika kwa maisha yao kutokana na utafiti unaofanywa na wataalamu pamoja na athari zinazoweza kujitokeza juu ya matumizi ya maji hayo yanayo dhaniwa kuwa na gesi.
Issa Mohamedi Kudekedela, mkazi wa kijiji hicho, ameelezea matumaini yake ya kupata huduma bora za afya ikiwemo umuhimu wa kujengewa zahanati ili kupunguza umbali wa kufuata huduma za afya.
Mwenyekiti wa kijiji, Rashidi Musa, amezungumzia kuhusu utafiti wa awali uliofanywa na wataalamu, akisema wamegundua viashiria vya gesi katika visima vyote viwili.
Aidha Rashidi Musa ameiomba serikali iendelee na utafiti zaidi ili wananchi waweze kuelewa mazingira yao na kuona jinsi gesi hiyo inaweza kusaidia kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili.
Mkuu wa wilaya ya Mtwara, Abdala Mwaipaya, amewahakikishia wananchi kuwa matumizi ya maji hayo ni salama na kuwataka kuwa watulivu wakati wataalamu wakiendelea na utafiti na mara itakapothibitishwa uwepo wa gesi asilia, wananchi watafaidika kupitia miradi ya maendeleo, ikiwa ni pamoja na kujengewa zahanati.