Biteko ataka siasa za kistaarabu uchaguzi serikali za mitaa
18 November 2024, 11:15 am
November 27,2024 kote nchini kunatarajiwa kufanyika kwa uchaguzi wa serikali za mitaa zitakazo waweka madarakani wenye viti wa vijiji,vitongoji,mitaa na wajumbe ambapo katika michakato ya awali ikiwa tayari imeshafanyika huku ikisubiriwa November 20 wagombea waanze kufanya kampeni.
Na Musa Mtepa
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko, amewataka wananchi wa Msimbati na Watanzania kwa ujumla kuwa na siasa za kistarabu katika kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa. Akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Msimbati, Novemba 17, 2024, baada ya kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo, Dkt. Biteko amesisitiza kuwa ni muhimu kwa wagombea kutangaza sera za maendeleo zitakazovutia wananchi kufanya maamuzi ya busara.
Katika ziara hiyo, Dkt. Biteko amekagua mradi wa ujenzi wa Kituo cha Afya, Kituo cha Polisi, na ujenzi wa taa za barabarani, akisisitiza kwamba miradi hiyo ni sehemu ya juhudi za kuboresha maisha ya wananchi. Aidha Dkt.Biteko ameongeza kuwa vyama vya siasa visiwafanye wananchi kuwa maadui, kwani serikali inatamani kuona mabadiliko chanya, hasa katika maeneo yenye rasilimali kama gesi asilia.
Diwani wa Kata ya Naumbu, Mh. Ali Hassani Mtima, amekubaliana na kauli ya Naibu Waziri Mkuu, akisisitiza umuhimu wa kuwa na uchaguzi wa kistarabu na kuwaomba wananchi kujitokeza kwa wingi siku ya uchaguzi ili kumchagua kiongozi wanayemtaka.
Wananchi wa Msimbati,Bi Anjela Boniface Milanzi, amekubaliana na wito wa kufanya kampeni za kistaarabu, huku akisisitiza kuwa viongozi wa kisiasa wanapaswa kutumia lugha ya busara ili kuepuka migogoro na kuhakikisha wanavutia wananchi kuchagua viongozi bora.