Nuru FM

Wilaya Ya Manyoni Yafikia Asilimia 90 Ya Zoezi La Anwani Za Makazi

20 April 2022, 7:19 am

HALMASHAURI ya Wilaya ya Manyoni imefikisha asilimia 90 ya zoezi la anwani za makazi na postikodi licha ya kuwepo changamoto ndogondogo zilizojitokeza.

Hayo yameelezwa na Mkuu wa Wilaya hiyo Rahabu Mwagisa wakati akitoa taarifa ya zoezi hilo kwa Mkuu wa Mkoa wa Singida Dk.Binilith Mahenge alipokuwa katika ziara ya kukagua zoezi hilo aliyoifanya leo wilayani humo.

“Tulikuwa na changamoto ya ukasanyaji wa  takwimu wakati wa uhainishaji wa hesabu ambapo awali tulipata idadi ya anwani za makazi 99,930 lakini baada ya kufanya masahihisho ya makadirio ya anwani tumebaini idadi kamili ni 42,000 kama zilizowasilishwa awali na watendaji wa kata ambao walihesabu idadi ya kaya badala ya anwani na katika utekelezaji ilibainika  kwamba kaya zaidi ya moja kuwa ndani ya anwani moja na kupelekea idadi ya anwani kuwa chache kuliko makadirio” alisema Mwagisa.

Akizungumza baada ya kupokea taarifa hiyo Dk.Mahenge aliitaka halmashauri hiyo  kuhakikisha zoezi hilo linakamilika kabla ya muda uliopangwa ili kwenda sambamba na wilaya zingine ambapo alitumia nafasi hiyo kuwapongeza viongozi wote kwa uchapaji kazi mzuri.

“Mkuu wa wilaya, mkurugenzi, mwenyekiti wa halmashauri, watumishi na wataalam wote kwa ujumla nitumie nafasi hii kuwapongezeni kwa kazi nzuri mnayoifanya kwa kushirikiana na wananchi na watendaji wenu” alisema Mahenge.

Dk. Mahenge alisema alisema zoezi hilo kimkoa limefikia asilimia 84.82 huku anwani za makazi zilizohesabiwa Singida Manispaa zikiwa ni 47,952, Ikungi 55,765, Iramba 55,686, Singida DC 50,672, Mkalama 45,039 na Itigi 35,000.

Wakati huo huo Dk. Mahenge amemtaka Mkandarasi wa Kampuni ya Luba Contractors CO.LTD ambayo imepata kazi ya kujenga jengo la wagonjwa mahututi na ujenzi wa wodi ya dharura (EMD) katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Singida ya Mandewa kukutana naye Aprili 25, 2022 ili kujadili kusuasua kwa ujenzi wa majengo hayo ambayo licha ya kupewa fedha bado ujenzi wake haujafika hata kiwango cha lenta huku kukiwa na sababu mbalimbali.

“Katibu Tawala nahitaji kuonana na mkandarasi mwenyewe hapa eneo la mradi ili tujadili atamalizaje hii kazi ndani ya muda aliopangiwa vinginevyo tutamnyang’anya huu mradi na kumpa mtu mwingine na pia tuna uwezo wa kumzuia hasipate kazi mahali popote hapa nchini” alisema Mahenge akioneshwa kukerwa na ucheleweshwaji wa ujenzi wa majengo hayo.

Aidha Mahenge alimtaka msimamizi wa ujenzi wa mradi huo kuhakikisha anafanya kazi usiku na mchana ukizingatia kuwa amewekewa taa kwa ajili ya kazi hiyo.

Katika ziara hiyo pia Dk.Mahenge alitembelea na kukagua ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Mkoa ya Wasichana ya Solya ambao ujenzi wake utagharimu Sh. 3. Bilioni ambayo inajengwa wilayani Manyoni.