Wazazi, walezi Katavi watakiwa kuwafundisha maadili mema watoto
29 September 2024, 8:36 am
“Walimu pamoja na wazazi wanatakiwa kuweka ulinzi mkubwa kwa Watoto ili kujenga taifa moja litakalokuwa na kizazi chenye maadili mema.”
Na John Mwasomola -Katavi
Wazazi na walezi mkoani Katavi wametakiwa kuwalinda watoto na kuwafundisha maadili yanayofaa ili kuwaepusha na vishawishi mbalimbali.
Wito huo umetolewa na Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Katavi Kaster Ngonyani wakati wa uzinduzi wa kampeni ya tuwaambie kabla hawajaharibiwa iliyofanyika katika viwanja vya Polisi Buzogwe mkoani Katavi.
Ngonyani amesema kuwa jeshi la polisi kwa kushirikiana na dawati la jinsia, walimu pamoja na wazazi wanatakiwa kuweka ulinzi mkubwa kwa watoto ili kujenga taifa moja litakalokuwa na kizazi chenye maadili mema.
Kwa upande wake Mkaguzi wa Polisi Judith Mbukwa ambaye ni Mkuu wa Dawati la Jinsia na Watoto Mkoa wa Katavi amewaasa wananchi kutoogopa kwenda kutoa taarifa za matukio yanayohusiana na ukatili wa kijinsia kwa kuwa hiyo ndiyo kazi ya jeshi la polisi kushirikiana na wananchi kutokomeza vitendo hivyo.
Mmoja wa wanafunzi ambao wameshiriki katika kampeni hiyo amewasihi wazazi kutowafanyia watoto vitendo vya kikatili ili kufanikiwa katika mambo yao, pia amewataka watoto kuendelea kujiamini na kutokubali kushawishika.
Mkuu wa Mkoa wa Katavi Mwanamvua Mrindoko ambaye alikuwa mgeni rasmi ametumia fursa hiyo kuwataka wazazi na walezi kuwa makini na watoto wao juu ya matumizi ya simu kwani baadhi yao wanajifunza matendo yasiyofaa kupitia simu zao.
Kampeni ya tuwaambie kabla hawajaharibiwa ni kampeni ya nchi nzima ambapo katika mkoa wa Katavi kampeni hiyo imefanyika katika viwanja vya Polisi Buzogwe na mgeni rasmi alikuwa Mkuu wa Mkoa Mwanamvua Mrindoko.