Nuru FM

Majangili Wanaswa na Meno ya Tembo

3 March 2023, 4:46 pm

Kamanda wa polisi mkoa wa Iringa ACP Allan Bukumbi na Kamishna Msaidizi hifadhi ya taifa Ruaha ACC Godwell Ole Meing’ataki wakionesha baadhi ya meno ya tembo.

Hii ni moja ya mafanikio ya misako inayofanyika na jeshi la polisi mkoa wa Iringa wakishirikiana na TANAPA.

Na Adelphina Kutika.

Askari wa Hifadhi ya Taifa ya Ruaha (Runapa) kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi Tanzania limewakamata watu watatu mjini Iringa wakiwa na meno nane mazima ya tembo na vipande sita yenye thamani ya zaidi ya Sh milioni 206.

Watuhumiwa hao ni pamoja na Greyson Lusasi (39) mkazi wa mtaa wa Mwangata mjini Iringa, Elia Halamga (55) mkazi wa Kateshi Manyara na Henry Chengula (38) mkazi wa mtaa wa Isakalilo Iringa mjini.

Akizungumza na wanahabari Mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Ruaha, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi Godwell Ole Meing’ataki amesema watuhumiwa hao walinaswa baada ya kupokea taarifa kutoka kwa wasamaria wema zilizoeleza uwepo wa mitandao ya ujangili na biashara ya nyara za serikali.

Mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Ruaha, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi Godwell Ole Meing’ataki akielezea tukio hilo.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa Kamishna Msaidizi wa Polisi, Allan Bukumbi amesema watuhumiwa hao walikamatwa Februari 28, mwaka huu majira ya saa 2.30 usiku katika mtaa wa Bombambili Mawelewele mjini Iringa.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa Kamishna Msaidizi wa Polisi, Allan Bukumbi akieleza walivyofanikisha kuwakamata wahalifu.

Pamoja na meno hayo ya tembo, amesema watuhumiwa hao waliokuwa katika gari aina ya Noah yenye namba za usajili T385 BWG walikutwa pia na jambia moja, msumemo mmoja mifuko ya sulphate mitatu iliyokuwa na meno hayo.

Amesema watuhumiwa hao watakaofikishwa mahakamani hivikaribuni baada ya upelelezi kukamilika walikamatwa wakiwa katika harakati za kutaka kufanya biashara na watu waliokuwa wakiwasiliana nao.