Nuru FM

Tuhuma,Muuguzi Kutumia Sindano Iliyotumika

22 February 2023, 12:04 pm

Kufuatia malalamiko kuhusu Mhudumu wa afya katika Zahanati ya Kijiji cha Tungamalenga,Johavina Mjuni anayedaiwa kutokuwa na huduma nzuri kwa wagonjwa.

Na Hawa Mohammed.

Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Iringa Limeagiza kufanyika uchunguzi wa haraka dhidi ya Mhudumu wa afya katika Zahanati ya Kijiji cha Tungamalenga, anayedaiwa kutokuwa na huduma nzuri kwa wagonjwa ikiwa ni pamoja na kutumia sindano iliyotumika kumtibu mgonjwa.

Akitoa agizo hilo kwa Idara ya afya katika kikao cha Baraza la Madiwani Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa vijijini Steven Mhapa amesema suala hilo linapaswa kufanyiwa kazi haraka kwa kuwa linahatarisha maisha ya watu.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa vijijini Steven Mhapa akitoa agizo.

Awali Diwani wa viti maalum tarafa ya Idodi Wilayani Iringa Shani Msambusi aliwasilisha  malalamiko hayo katika Baraza la Madiwani na kumtaja mhudumu huyo wa afya aliyefahamika kwa jina la Johavina Mjuni kuwa ni kero kwa wananchi wanaopata huduma katika Zahanati hiyo kutokana na utovu wa nidhamu uliokithiri na kushindwa kufanya kazi kwa weledi.

Diwani wa Viti Maalum tarafa ya Idodi Wilayani Iringa Shani Msambusi akiwasilisha  malalamiko hayo katika Baraza la Madiwani.

Kufuatia malalamiko hayo Kaimu Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa Dkt. Luvanda Witson alisema wanaanzisha uchunguzi wa haraka dhidi ya madai hayo na pindi watakapojiridhisha hatua za kinidhamu zitachukuliwa  na kulijulisha baraza la madiwani kuhusu hatua hizo.

Kaimu Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa Dkt. Luvanda Witson akieleza mkakati wa kuchanganua kadhia hiyo.