Nuru FM

watahiniwa 2194 wafutiwa matokeo ya mtihani wa darasa la saba

1 December 2022, 9:55 am

Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA) leo limetangaza matokeo ya darasa la saba kwa mwaka 2022 ambapo limetangaza kufuta matokeo yote ya Watahiniwa 2,194 sawa na asilimia 0.16 ya Watahiniwa waliofanya mitihani.

NECTA imefikia uamuzi huo siku chache baada ya zaidi ya watahiniwa 1,350,881 waliofanya mtihani ambao wamebainika kufanya udanganyifu katika mtihani huo wa kumaliza elimu ya msingi mwaka 2022.

Akitangaza matokeo ya mtihani wa kumaliza darasa la saba mwaka 2022, Kaimu Katibu Mtendaji wa Necta, Athuman Amasi  amesema pia NECTA imezifungia shule 24 kuwa vituo vya mitihani ya Taifa baada ya kuthibitika kupanga kufanya udanganyifu katika mitihani ya kumaliza elimu ya msingi.

Shule hizo ambazo ni sawa na asilimia 0.13 ya vituo vyote vya mitihani nchini, ndani yake zipo shule maarufu ikiwemo ya Musabe ya jijini Mwanza na St Anne Marie ya jijini Dar es Salaam na shule ya Rweikiza ya mkoani Kagera.

Shule hizo ni Kadama shule ya msingi iliyopo Chato- Geita, Rweikiza (Bukoba), Kilimanjaro shule ya msingi (Arusha) Sahare (Tanga), Ukerewe (Mwanza), Peaceland (Mwanza), Karume (Kagera), Al-hikma (Dar es Salaam), Kazoba (Kagera), Mugini (Mwanza), Busara (Mwanza), Jamia (kagera), Winners (Mwanza), Musabe (Mwanza), Elisabene (Songwe), High Challenge (Arusha), Tumaini (Mwanza), Olele (Mwanza), Mustlead (Pwani).