Nuru FM

Sh .Bilioni 1.7 Za Uviko_19 Zakamilisha Mradi Wa Jengo La Madarasa, Maabara Na Ofisi Chuo Cha Ufundi Arusha

11 September 2022, 3:42 pm

Fedha za Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya UVIKO 19 zaidi ya bilioni 1.7 imewezesha kukamilishwa kwa Mradi wa jengo la madarasa, maabara na ofisi katika Chuo cha Ufundi Arusha (ATC)

Akitoa taarifa ya utekelezaji wa Mradi huo kwa Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Huduma na Maendeleo ya Jamii leo Septemba 11, 2022, Mkuu wa Chuo hivho Dkt. Mussa Chacha amesema kukamilika kwa mradi huo kutawezesha kupunguza changamoto ya msongamano wa wanafunzi na wanataaluma na mtundikano wa ratiba za masomo.

Ameongeza kuwa Mradi huo ambao una madarasa nane, maabara sita na ofisi 26 una uwezo wa kuhudumia wanafunzi 1,025 na wanataaluma 104 kwa wakati mmoja na kwamba mpaka kukamilika utakuwa umegharimu shilingi bilioni tano.

“Kwa sasa kumekuwa na upungugu wa madarasa, ofisi za wanataaluma, hivyo kukamilika kwa mradi huu kutapunguza chngamoto ambazo zimekuwapo kuyokana na upungufu wa majengo haya” amesema Dkt Chacha.

Ameongeza kuwa tayari Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imeshatoa zaidi ya milioni 481 kwa ajili ya kununua na kuweka samani katika jengo hilo linalotarajiwa kuanza kutumika mwishoni mwa mwezi septemba.

Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Huduma na Maendeleo ya Jamii Mhe. Stanslaus Nyongo (Mb) ameipongeza Wizara kwa usimamizi mzuri wa Mradi huo ambapo amesema thamani ya fedha iliyotumika katika jengo hilo inaonekana.

“Jengo hili limejengwa kwa viwango na ubora, thamani ya frdha inaonekana naipongeza wizara kwa kusimamia fedha zilizowekwa katika mradi huu” amesema Nyongo.

Aidha, amewataka watumishi wa umma wanaopewa dhamana ya kusimamia na kutekeleza miradi ya serikali kuwa wazalendo na kuthamini nafasi wanazopewa ili kuleta tija katika shughuli wanazofanya.