Nuru FM

Mkemia Mkuu wa Serikali aonya matumizi holela ya madawa

15 May 2022, 1:08 pm

Mkemia Mkuu wa Serikali Daktari Fidelis Mafumiko ameionya jamii kuepuka ununuzi na matumizi holela ya dawa zisozosajiliwa wala kuthibitishwa na mamlaka husika ikiwemo kuangalia aina za viambata au kemikali zilizotumika katika kutengeneza dawa hizo.

Dk. Mafumiko ameyasema hayo alipotembea banda la Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali katika maonesho ya tano ya mifuko na programu za uwezeshaji wananchi kiuchumi yaliofanyika katika viwanja vya Jamuhuri mkoani Morogoro.

Amesema matumizi holela ya dawa yanaweza kumsababisha mtu kupata madhara ya kiafya kutokana na kushindwa kufahamu aina ya kemikali zilizotumika kutengeneza dawa hizo.


Dkt. Mafumiko amewataka wananchi kununua dawa zilizothibitishwa na mamlaka husika kwa kuwa ni halali kwa matumizi ya biaadamu au wanyama.

Aidha amewataka wajasiriamli wakubwa,wadogo pamoja na wananchi kwa ujumla kutumia fursa ya maonesho mbalimbali yanayoandaliwa na serikali katika maeneo tofauti hapa nchini kufika katika banda la Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kuweza kupata elimu juu ya matumizi sahihi ya kemikali katika bidhaa zao wanazozizalisha.

Amewataka wajasiriamali nchini kufuata kanuni za matumizi sahihi ya kemikali wanazozitumia hasa tindikali (acid ) katika kutengeneza bidhaa zao ili kuepuka madhara yanayojitokeza kutokana na matumizi holela ya kemikali hizo.