Nuru FM

Wananchi Lulanzi Wilaya Ya Kilolo Wakamilisha Kuchimba Mfereji Wa Kupeleka Maji Kwa Walemavu

14 May 2022, 9:07 am

Wananchi wa kijiji cha lulanzi  Wilaya ya Kilolo wamekamilisha kuchimba Mfereji wa kupeleka huduma ya maji ya bomba katika familia ya watu watatu wenye ulemavu.

Akizungumza na Nuru fm mara baada ya kukamilisha kuchimba mfereji huo Mwenyekiti wa kijiji hicho Bw Lucas Kihongosi amesema kuwa wananchi wake wamekamilisha zoezi hilo kwa kutoa nguvu kazi ili kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Balozi wa utalii nchini Tanzania Isabella Mwampamba kwa kushirikiana na serikali Wilaya ya Kilolo, Umoja wa wanawake watalii Nyanda za juu kusini pamoja na wadau wa maendeleo.

Kwa upande wake Balozi wa Utalii Nchini Isabella Mwampamba amesema kuwa zoezi linalofuata mara baada ya mfereji huo kukamilika ni kutandaza mabomba ambapo mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira Iruwasa Kanda ya Wilaya ya Kilolo itaanza zoezi hilo mara moja.

Amesema kuwa gharama za kupeleka maji ya bomba katika familia hiyo ni miongoni mwa mafanikio ya harambee ambayo ilifanyika katika ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Kilolo tarehe 5/5/2022 ambapo katika harambee hiyo Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Kassim Majaliwa Majaliwa alichangia kiasi cha shilingi Milion 5 kati ya shilingi milioni 10 zilizopatikana siku hiyo.

Hata hivyo walemavu hao wana uhitaji wa kuvutiwa maji, kujengewa nyumba ya kisasa, kupatiwa vifaa vya malazi, vifaa vya jikoni na gharama za chakula matibabu ambapo gharama zote ni shilingi milioni 20 na FEDHA zote zinapolokelewa kupitia acaount namba ya CRDB iliyosajiliwa kwa jina la Isabella African Foundation ya 015C621885600 huku Miradi hiyo ikitarajiwa kukamilika kwa muda wa miezi mitatu kuanzia mwezi Mei mpaka Julai 2022.

Awali Mwenyekiti wa Kamati ya wanawake watalii Mkoa wa iringa Lilian Mbedule ambao walikuwa na wazo la kuwatembelea walemavu hao ameahidi kushirikiana kuhakikisha walemavu hao wanapata mahitaji yote muhimu kama walivyopanga.

Aidha amesema kuwa  Umoja wa wanawake watalii Nyanda za juu kusini unatarajia kufanya harambee kubwa mkoani iringa mwezi wa sita yenye lengo la kukusanya fedha zitakazosaidia kutatua changamoto zinazowakabili walemavu hao ukiwa ni muendelezo wa utalii wa kujitolea kwa kurudisha kwa jamii.