Nuru FM

Jeshi la Polisi Dar laimarisha usalama mechi ya Yanga vs Simba Jumamosi

29 April 2022, 9:39 am

Kamanda wa Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es salaam Kamishana Msaidizi Mwandamizi wa Polisi Jumanne Muriro amewatoa hofu Mashabiki wa Soka wa Simba SC na Young Africans ambao timu zao zitakutana kesho Jumamosi (April 30), Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Kamanda Muriro amesema Mashabiki wa Soka na Wananchi wa Mkoa wa Dar es salaam wanapaswa kuwa na amani kuelekea mchezo huo, kwani Jeshi la Polisi limejipanga ipasavyo kuhakikisha hali ya amani inaendelea muda wote kabla, wakati na baada ya mchezo.

Kamanda Muriro amesema jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es salaam linatambua uwepo wa mchezo huo Mkubwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara, ambao utachezwa Uwanja wa Benjamin Mkapa kuanzia saa kumi na moja jioni.


Amesema Jeshi la Polisi limejipanga kisawasawa ili kuhaklikisha Mashabiki na wananchi wengine wanaendelea kuwa na amani wakati wote, hivyo ametoa onyo kwa wenye nia mbaya ya uvunjifu wa amani.

“Tunatambua uwepo wa mpambano huo wenye upinzani wa jadi, tunajua timu hizi zina mashabiki wengi na wamejipanga kwenda Uwanja wa wa Mkapa kuzishuhudia timu zao zikicheza, hivyo basi Jeshi la Polisi limejipanga kuhakikisha hali ya usalama kwa Wananchi inakuwepo wakati wote.”

“Tumejiandaa vizuri kuhakikisha kwamba, masuala ya kiusalama ndani na nje ya Uwanja wa Mkapa yanaimarishwa, na wapenzi wote tutahakikisha wanafuata taratibu na sheria za mchezo wa Soka katika kuingia uwanjani hapo.”

“Vitu vyote ambavyo vina mahusiano ya silaha (Silaha za moto na silaha zisizo za moto – CHUPA- VISU- MAPANGA), havitaruhusiwa kuingia au kuwepo kwenye sehemu ya wapenzi watakaokuwa majukwaani.” amesema Kamanda Muriro.

Young Africans kesho itaingia Uwanja wa Benjamin Mkapa huku ikiwa inaongoza msimamo wa Ligi Kuu kwa kufikisha alama 54 ambazo zinawapa nafasi kubwa ya kutwaa ubingwa wa Tanzania Bara msimu huu 2021/22.

Simba SC inayotetea ubingwa inashika nafasi ya pili kwenye msimamo huo, ikiwa na alama 41, ambazo zinaifanya kuwa nyuma kwa alama 13 dhidi ya Young Africans