Katavi: Wanaume wanaotelekeza familia baada ya mavuno waonywa
2 July 2024, 6:07 pm
Picha inaonyesha baadhi ya mazao yanayolimwa kwa wingi mkoani Katavi ikiwemo mahindi mpunga na karanga.
“Tabia ya baadhi ya wanaume kutelekeza familia zao hasa baada ya kipindi cha mavuno zinasababisha ukatili katika jamii.“
Na Fatuma Saidi -Katavi
Jamii imeaswa kuacha tabia ya kutelekeza familia zao hasa kipindi cha mavuno jambo linalopelekea uwepo wa matukio mbalimbali ikiwemo mauaji na ukatili wa kijinsia ambao hutokea kwa baadhi ya familia mkoani Katavi.
Akizungumza na Mpanda Radio FM afisa wa polisi kitengo cha dawati la jinsia mkoani Katavi, Emmanuel Thobias ameeleza kuhusu tabia ya baadhi ya wanaume wanaotelekeza familia zao hasa baada ya kipindi cha mavuno.
Emmanuel amesema kuwa kitendo cha utelekezwaji wa familia hupelekea baadhi ya wanawake kushindwa kuvumilia hali hiyo na kusababisha kuibuka kwa matukio ya mauaji na migogoro katika familia .
Hata hivyo amesema kuwa ifikapo kipindi cha mavuno familia nyingi hutengana kutokana tabia ya baadhi ya wanaume kuingia tamaa ya kuongeza mke mwingine na hivyo kupelekea watoto kukosa malezi yaliyo sahihi kutoka wazazi wao.