Wabeba taka Mpanda wameshindwa kazi?
20 February 2024, 5:24 pm
Wananchi wamesema mtaa huo umekuwa na harufu kali ambayo imekuwa haivumiliki na wamekosa namna ya kufanya hivyo wanahifadhi kwenye mifuko kwa sababu taarifa za taka hizo wamelalamika kwa viongozi wao bila mafanikio yeyote.
Na Samwel Mbugi-Katavi
Wananchi wa kata ya Majengo mtaa wa Paradise Manispaa ya Mpanda mkoa wa Katavi wamesema takataka zimekuwa kero kubwa katika mtaa huo na kusababisha funza kuingia ndani ya nyumba zao wanazoishi.
Hayo yamesemwa na wananchi walipokuwa wakizungumzana Mpanda Radio Fm katika mtaa huo ambapo wamesema kwa muda mrefu kumekuwa na mrundikano wa taka kwenye mifuko bila kutolewa na mamlaka zinazohusika na uzoaji.
Wananchi wamesema mtaa huo umekuwa na harufu kali ambayo imekuwa haivumiliki na wamekosa namna ya kufanya hivyo wanahifadhi kwenye mifuko kwa sababu taarifa za taka hizo wamelalamika kwa viongozi wao bila mafanikio yeyote.
Hata hivyo mwenyekiti wa mtaa huo Magireth Atanasi amekiri kuwepo kwa Mrundikano wa taka kwenye mtaa huo, ambapo amesema viongozi wanaohusika na uzoaji wa taka hizo wamekuwa wakitoa ahadi ambazo hazitekelezeki kwa muda mrefu.
Afisa Mazingira wa manispaa Alex Semwali amesema ni kweli changamoto hiyo ipo lakini wiki hii wanafanya jitihada za kuzoa taka hizo zilizopo kwenye makazi ya wananchi.
Kadhalika Semwali ameongeza kwa kusema changamoto iliyopelekea mrudikano mkubwa wa taka kwenye makazi ya wanachi ni uhaba wa magari ya kubebea taka hizo.