Nuru FM

wazee 54 wameripotiwa kuuawa nchini kwa imani za kishirikina

11 June 2022, 8:25 am

Kwa mujibu wa jeshi la Polisi katika kipindi cha Januari hadi Desemba mwaka 2020 kulikuwa na matukio 54 ya kuuawa kwa wazee nchini, lakini katika kipindi cha Januari hadi Desemba, 2021 hapakuwepo na tukio lolote la kuuawa kwa wazee nchini.

Aidha, kwa kipindi cha Januari hadi Juni, 2022 kumetokea matukio kwenye  Mkoa wa Singida, Wilaya ya Iramba la mauaji ya wazee watatu (3) wanawake kwa kuhusishwa na imani za kishirikina, hii haikubaliki, alisisitiza Dkt. Gwajima.

Waziri wa Maendeleo ya Jamii Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Dorothy Gwajima ametoa kauli hiyo Juni, 10, 2022, jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa Habari kuelekea Siku ya kupinga ukatili kwa Wazee Duniani itakayo adhimishwa  Juni 15, 2022.

Dunia inaadhimisha  Siku ya Kimataifa ya Kupinga Ukatili dhidi ya Wazee ambapo Siku hii huadhimishwa kufuatia Azimio la Umoja wa Mataifa Na. 66/127 la Desemba 2011 lililotokana na maombi ya Shirika la Mtandao wa Kimataifa wa Kuzuia Ukatili dhidi ya Wazee.

Waziri huyo ameitaka jamii kulikumbuka kundi la Wazee wakati wa Sensa ya Watu na Makaazi itakayofanyika  Agosti 23, 2022 ili nao waweze kuingizwa kwenye mipango ya taifa.

Ameongeza kuwa Nikupitia takwimu za Sensa pekee ndio zitaweza kusaidia kupanga mipango mizuri ya nchi, hivyo tunapokwenda kuadhimisha siku hii iliyobebwa na kaulimbiu “Tuhakikishe wazee wanalindwa, wanasikilizwa na kuheshimiwa, tusikose kuhesabiwa kwenye Sensa ya Watu na Makazi.

“Ni imani yangu kila mmoja kwa nafasi yake atakuwa msatari wa mbele kuhimiza zoezi la sensa ka makundi yote likiwepo kundi hili la wazee” amesema Dkt. Gwajima

Amesema lengo la maadhimisho hayo ni kuelimisha jamii kuhusu kupinga ukatili wa aina zote dhidi ya Wazee ambao ni ukatili wa kimwili, kihisia na kiuchum sambamba na kuelimisha jamii juu ya changamoto mbalimbali zinazowakabili Wazee zinazotokana na mila na desturi potofu, fursa walizonazo na masuala ya uzee na kuzeeka.

Dkt. Gwajima amefafanua kuwa katika kukabilina na changamoto hiyo Serikali imeunda mabaraza ya wazee kuanzia ngazi ya kijiji hadi Taifa ambapo yako takribani 20,749, mabaraza hayo kwa kushirikiana na wadau ili yatumike kutoa elimu kuhusu ukatili dhidi ya wazee.

Katika hatua nyingine Waziri Dkt. Gwajima, ameitaka jamii, kuendelea kujiunga kwenye kampeni  ya SHUJAA WA MAENDELEO NA USTAWI WA JAMII (SMAUJATA) kupitia kiungio cha https://forms.gle/DtGthrUTLhXJp2cUA  pia kwenye mtandao wa kijamii wa Telegram kwa link; https://t.me/+IFypK6_FB-k30TIk. Kwa upande wa Instagram ni @smaujata.tz.