Nuru FM

Wakazi wa Lulanzi wajitolea kuchimba mtaro wa kupeleka maji kwa familia yenye walemavu watatu

6 May 2022, 7:31 am

Wakazi wa Kijiji cha lulanzi kilichopo Wilaya ya Kilolo Mkoani Iringa wameshiriki kuchimba mtaro wa kupeleka maji katika familia ya watu watatu wenye ulemavu ili kutatua changamoto ya huduma hiyo.

 

Wakizungumza mara baada ya kutembelewa na balozi wa utalii nchini Tanzania Isabella Mwampamba kujionea usanifu uliofanywa na Mamlaka ya maji na usafi wa Mzingira Iruwasa Kanda ya Wilaya ya Kilolo, baadhi ya wananchi hao wamesema kuwa wameamua kutoa nguvu kazi hiyo ili walemavu hao wapate maji safi ya bomba nyumbani kwao.

Katika kuhakikisha zoezi la kuchimba Mtaro linafanyika kwa ufanisi, wanawake wa kijiji hicho kwa kushirikiana na Diwani wa Kata hiyo Mh. Mkakatu waliahidi kutoa Mahindi, mchele, kuni, mafuta na Fedha ili waweze kuwapikia wanaume wa kijiji chao walioamua kufanya kazi hiyo.

 

Naye balozi wa utalii Nchini Bi Isabella Mwampamba alitoa kiasi cha shilingi laki moja ili ziweze kutumika kununua chakula na vinywaji kwa wananchi waliojitokeza kutoa nguvu kazi yao kuhakikisha walemavu hao wanapata huduma ya maji.

Kwa upande wake Mhandisi kutoka Mamlaka ya maji na usafi wa Mzingira Iruwasa Kanda ya Wilaya ya Kilolo Paulo Mboka amesema kuwa watahakikisha huduma ya maji inafika kwa familia hiyo yenye watu wenye ulemavu kwa muda mchache kutokana na wananchi wa kijiji cha Lulanzi kutoa nguvu kazi.

 

Naye Diwani wa Kata la Mtitu Mh. Mkakatu amewangeza wananchi wa kijiji cha Lulanzi kwa kutoa nguvu kazi hiyo huku akimshukuru balozi wa Utalii Isabella mwampamba kwa kuwa na moyo wa kuwaidia familia hiyo toka alipopata taarifa ya changamoto wanazopitia walemavu hao.

 

MWISHO