Mfungwa atuhumiwa kumbaka mtoto wa miaka 13 Katavi
5 March 2024, 3:13 pm
“Mkuu wa mkoa wa Katavi Mwanamvua Mrindoko amesema suala hilo lipo katika uchunguzi na hatua kali za kisheria zitachukuliwa huku wao kama serikali wamesikitishwa kutokea kwa tukio hilo”
Na Gladness Richard-Katavi
Binti mwenye umri wa miaka 13 mkazi wa kijiji cha Kawanzige kata ya Kakese manispaa ya Mpanda mkoani Katavi amebakwa na mfungwa wa gereza la Kalilankulunkulu wakati alipokuwa anatoka mbugani kupanda mpunga.
Binti huyo ambaye jina lake limehifadhiwa amesema kuwa tukio hilo limetokea wakati alipotoka mbugani akiwa na wenzake ndipo mfungwa huyo akiwa anachunga ng’ombe aliwaamuru wasimame na baadaye kufanya tukio hilo.
Kwa upande wake kaimu mganga mkuu wa hospitali ya manispaa ya Mpanda Limbu Mazoya amesema kuwa walimpokea binti huyo na baada ya kumfanyia uchunguzi alionekana kuwa na viashiria vya kubakwa.
Hata hivyo mkuu wa mkoa wa Katavi Mwanamvua Hoza Mrindoko wakati akizungumza na waandishi wa habari amesema suala hilo lipo katika uchunguzi na hatua kali za kisheria zitachukuliwa huku wao kama serikali wamesikitishwa kutokea kwa tukio hilo.
Mrindoko amesema matukio ya ukatili yamezidi kuwa mengi huku akiwaomba wazazi na walezi kutoyafumbia macho masuala ya ukatili na kuwataka watoe taarifa pindi matukio kama hayo yanapojitokeza.