Joy FM
Joy FM
17 March 2026, 11:08

Majiko banifu yamekuwa suluhisho muhimu katika kukabiliana na changamoto za kimazingira na kijamii katika nchi nyingi zinazoendelea, ikiwemo Tanzania na kwa muda mrefu jamii nyingi zimekuwa zikitegemea kuni na mkaa kama vyanzo vikuu vya nishati ya kupikia hali ambayo imesababisha uharibifu mkubwa wa mazingira pamoja na kuongeza mzigo kwa wanawake na wasichana kubakwa wakiwa wameenda kutafuta kuni.
Na Emmanuel Kamangu
Zaidi ya majiko banifu 400 yametolewa kwa wananchi wa kata sita za tarafa ya Buyonga Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu ikiwa ni utekelezaji wa ahadi ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan aliyoitoa kwa wananchi wakati akifungua Bunge la jamuhuri ya Muungano wa Tanzania na kuahidi ndani ya siku 100 za uongozi wake kuhakikisha watanzania wananufaika na matumizi ya nishati safi.
Mgeni rasmi wa hafla ya uzinduzi wa majiko banifu ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Kasulu Kanal Isack Mwakisu amewata wananchi kuyatumia katika njia sahihi inayolengwa na serikali ya utunzaji wa mazingira ikiwa ni pamoja na kumsaida mwananchi kuondokana na nishati isiyo salama.

Aidha Mkurugenzi Mtendaji wa Mtandao wa Wanawake Wajasiriamali Tanzania (TAWEN) Bi. Florence Masunga amesema kuwa Rais Dkt Samia amedhamiria kuondoa matumizi ya kupikia kuni Kampeni inayolenga kufikia mwaka 2036 kuhakikisha kila Mtanzania anapata nishati safi ya kupikia.

Kwa upande wao, baadhi ya wananchi wa Tarafa ya Buyonga ambao wamenufaika na majiko banifu mmoja wao akiwa Bi Husna Kagaruki wameishukuru serikali huku wakibainisha kuwa majiko hayo yanaenda kuwapunguzia gharama za maisha kwa kutumia mkaa kidogo.