Joy FM
Joy FM
24 June 2025, 15:52

Serikali na wadau wa maendeleo wameendelea kuwahimiza vijana kuwa wabunifu ili waweze kujiajiri kupitia bunifu mbalimbali.
Na Hagai Ruyagila
Wahitimu wa mafunzo ya ushonaji wa vazi maalumu la kulinia asali na teknolojia ya umeme jua katika chuo cha Veta Kasulu mkoani Kigoma wametakiwa kutumia ujuzi huo kujiingizia kipato ili kujikwamua kiuchumi.
Shirika la maendeleo nchi Ubelgiji Enabel, kwa kushirikiana na Chuo cha Veta Kasulu kupitia mradi wa “Wezesha Binti” imeendesha mafunzo hayo kwa kipindi cha wiki mbili kwa vijana wa kike na wakiume 104.
Katibu tawala wa wilaya ya Kasulu Bi. Theresia Mtewele, aliyekuwa mgeni rasmi wakati wa mahafari hayo amesema wanachuo hao wanapaswa kuyatumia mafunzo hayo kama chachu ya kujiingizia kipato kwa ajili ya maisha yao ya baadae.

Kaimu mkuu wa chuo cha Veta Kasulu Zacharia Mafwele amesema mahitaji yalikuwa makubwa na bajeti ilikuwa ndogo hivyo wadau wa maendeleo likiwemo shirika la Enabel wameombwa kuendelea kutoa msaada kwa jamii ili iweze kujikwamua kiuchumi.
Mwakilishi wa shirika la Enabel wilaya ya Kasulu Bw, Abel Mbilinyi amesema licha ya kujiingizia kipato amewasihi kuwa na nidhamu katika kazi wanayokwenda kuifanya.
Baadhi ya Vijana waliyohitimu katika mafunzo hayo wamesema elimu waliyoipata katika chuo hicho itawasaidia kujiingizia kipato nakuwa mfano wakuigwa katika jamii inayowazunguka.
