WPC yatoa baiskeli kwa vijana kukabiliana na mimba kwa watoto wa kike
7 November 2024, 16:55
Serikali katika Halmashauri za Wilaya Kibondo na Kakonko imesema itaendelea kushirikiana na wadau wa maendeleo ili kuwasaidia vijana mikopo inayotolewa kwa ajili ya kuhakikisha wanapata mafanikio kupitia shughuli mbalimbali na kuwaepusha na mimba za utotoni.
Na James Jovin – Kibondo
Shirika la women’s Promotion center WPC kupitia mradi wa KAGS limetoa jumla ya baiskeli 24 zilizogharimu shilingi million 7.5 kwa makundi mbali mbali ya vijana katika wilaya za Kibondo na kakonko ili kusaidia kuwafikia wasichana wanaopatwa na madhira mbali mbali ikiwemo kubebeshwa mimba lakini pia kusaidia familia masikini zinazojiingiza katika mikopo hatarishi.
Hayo yamebainishwa na Bi. Lilian Solile afisa mradi shirika la women’s promotion center wakati wa kugawa baiskeli hizo kwa makundi ya vijana katika wilaya za Kibondo na Kakonko ambapo mradi huo umekuwa ukitekelezwa katika kata sita ndani ya wilaya hizo mbili.
Kwa upande wake Bi. Martha Jerome ambaye ni mkurugenzi wa shirika la Women’s Promotion Center amesema kuwa shirika hilo pia limekuwa likitoa baiskeli kwa wasichana ambao wanatembea umbali mrefu kwenda kuitafuta elimu hali ambayo kwa kiasi kikubwa imepunguza adha hiyo kwa baadhi ya wasichana waliosaidiwa.
Baadhi ya vijana waliowezeshwa na shirika hilo kupitia mradi wa Kagis wameelezea mafanikio waliyofikia mpaka sasa mradi huo ukiwa na Zaidi ya miaka minne tangu kuanza kutekelezwa.
Naye Bw. Stephen Mabuga ambaye ni afisa maendeleo ya jamii wilaya ya Kakonko pamoja na bi. Jackline Isaack afisa maendeleo katika halimashauri ya Kibondo wamewataka vijana hao kuchangamkia piampo mikopo inayotolewa na halimashauri za wilaya ili kuendelea kupanua wigo wa kusaidia wasichana wenye changamoto na jamii kwa ujumla.