Idadi ya wanaojifungulia kwa wakunga wa jadi yapungua Kibondo
25 October 2024, 13:40
Serikali imesema itaendelea kuhamasisha wajawazito kuhakikisha wanajifungulia kwenye vituo vya kutolea huduma za afya ili kuendelea kupunguza vifo vya watoto wachanga na watoto.
Na James Jovin – Kibondo
Idadi ya akina mama wajawazito wanaojifungulia kwa wakunga ama waganga wa jadi imepungua kwa zaidi ya asilimia 97 katika kijiji cha Kibuye kata ya Kumsenga wilayani Kibondo mkoani Kigoma baada ya serikali kuboresha huduma za afya katika kijiji hicho katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita.
Wakizungumza na Redio Joy Fm, baadhi ya wananchi wakazi wa kijiji cha Kibuye wilayani Kibondo wamesema kuwa idadi kubwa ya akina mama wajawazito walikuwa wakilazimika kujifungulia kwa wakunga ama waganga wa kienyeji kutokana na umbali wa zaidi ya kilometa 30 kufuata huduma za afya huku hali ya uchumi ikiwa kikwazo kikubwa.
Kwa upande wake, afisa muuguzi katika zahanati ya Kibuye Alpha Tarimo amesema kuwa zahati hiyo kwa sasa baada ya kuboreshwa ina uwezo wa kupokea zaidi ya wajawazito 185 kwa mwaka hali ambayo inasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza idadi ya vifo vya akina mama wajawazito na watoto ambao wangefariki kwa kujifungulia kwa wakunga na waganga wa jadi.
Naye Mganga Mkuu wa Wilaya ya Kibondo Dkt. Henry Chinyuka amesema kuwa katika kupunguza ama kumaliza kabisa tatizo la akina mama wajawazito kujifungulia kwa wakunga ama waganga wa jadi serikali imeanzisha huduma ya M- MAMA ambapo mama mjamzito mahali popote alipo hasa vijijini anaweza kusafirishwa bure mpaka katika zahanati iliyo karibu ama kituo cha afya.
Katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita idara ya afya katika halimashauri ya wilaya ya Kibondo imepokea zaidi ya shilingi bilioni 2.9 ili kuboresha miundombinu mbalimbali na kuongeza vifaa tiba lakini pia upande wa huduma za akina mama wajawazito na watoto wachanga.