Tbs na Sido watoa mafunzo Kwa wasindikaji na wazalishaji wa Mpunga.
22 March 2023, 10:50 am
KATAVI
Serikali kupitia Shirika la viwango Tanzania TBS kwa kushirikiana na shirika la kuhudumia viwanda vidogo SIDO limeanza kutoa mafunzo kwa wasindikaji na wazalishaji wa zao la mpunga mkoani Katavi lengo likiwa ni kuongeza uzalishaji na ubora wa bidhaa za chakula zitokanazo na mchele.
Akizungumza kaimu meneja wa TBS kanda ya juu kusini Rodney Alananga pamoja na kaimu meneja SIDO SalomeCharles wamesema kuwa lengo kuu la mafunzo hayo ni kutoa picha ya soko la afrika lilivyo na kuwafundisha namna ya kulifikia soko kwa kuzalisha na kusindika bidhaa kulingana na soko la sasa.
Aidha washiriki wa mafunzo hayo ambapo ni wazalishaji na wasindikaji wa zao la Mpunga wameishukuru serikali kwa kuwaletea mafunzo hayo kwani yatawasaidia kukuza thamani ya zao la Mpunga Katavi na Tanzania kwa ujumla.
Awali akifungua mafunzo hayo Mgeni rasmi aliyemwakilisha mkuu wa mkoa wa Katavi Mwanamvua Mrindoko, Onesmo Buswelu ambaye pia ni mkuu wa wilaya ya Tanganyika amesema mafunzo hayo yaambatane na zoezi la upandaji wamiti ili kutunza mazingira na kuwataka washiriki wayazingatie watakayoyapata kwaajili ya kukuza uchumi wa mkoa na Taifa.
Mafunzo hayo yatafanyika mkoani Katavi kwa muda wa siku kumi katika Wilaya ya Mpanda, Tanganyika, Mlele na Nsimbo.