Vijana Waaswa Kuchangamkia Fursa za Mikopo ya Halmashauri
16 February 2023, 4:47 am
TANGANYIKA
Vijana Halmashauri ya wilaya ya Tanganyika mkoani Katavi wametakiwa kutumia fursa ya mikopo ya asilimia nne ili kujikwamua kiuchumi.
Hayo yamesemwa na Mjumbe wa baraza kuu la UVCCM Mkoa wa Katavi Mhandisi Debora Joseph katika kikao cha baraza kilichofanyika kijiji cha Majalila amesema kuwa pamoja na serikali kuwa na mpango wa kutoa fedha za mikopo kwa vijana kupitia asilimia 4 baadhi ya vijana wamekuwa wakikosa uaminifu wa kutorudisha fedha hizo.
Aidha akitoa taarifa ya utoaji wa mikopo katika Halmashauri ya wilaya ya Tanganyika Afisa Maendeleo ya jamii Halima Kitumba amesema wameendelea kutoa mikopo hiyo licha ya kuwepo kwa changamoto ya ulejeshaji ambapo hadi sasa jumla ya shilingi milioni 318 hazijarejeshwa na vijana tangu 2009.
Kwa upande wao baadhi ya vijana wamesema wamekuwa wakifuata utaratibu wa kuomba mikopo hiyo huku baadhi yao wakipata na wengine kukosa fursa hiyo kwa masharti ya kukosa vigezo.
Katika kukabiliana na changamoto ya uchumi kwa vijana serikali ilikuja na mpango wa kuwakopesha vijana asilimia nne ya mapato ili kujikwamua kiuchumi.