Mwanamke akutwa amejinyonga kijiji cha Magamba
21 January 2025, 4:52 pm
Picha ya Kamanda wa polisi mkoa wa Katavi. Picha na Anna Milanzi
“Mwanamke mmoja akutwa amefariki dunia kwa kujinyonga na kanga yake”
Na Leah Kamala
Mwanamke mmoja anaesadikiwa kuwa na umri kati ya miaka 19 hadi 22 ambaye jina lake halijafahamika amekutwa amefariki dunia kwa kujinyonga
Taarifa inaeleza kuwa mwili wa marehemu umekutwa ukuning’ing’inia juu ya mti katika kitongoji cha Makongolo kilichopo kata ya Magamba manispaa ya Mpanda mkoani katavi .
Akizungumzia tukio hilo mwenyekiti wa kijiji cha Makongolo Zeno Saidi amebainisha kupokea taarifa kutoka kwa watoto wanaochunga ng’ombe juu ya uwepo wa mwili wa binti huyo ukiwa umening’inia kwenye mti huku akiwa ana majeraha katika miguu.
Kwa upande wao baadhi ya mashuhuda wa tukio hilo wamesema kuwa binti huyo ni mgeni katika eneo hilo ambapo wameiomba serikali iweze kuendelea kutoa elimu kwa wananchi wasichukue maamuzi yasiyofaa na huku wakilitaka jeshi la polisi kufanya uchunguzi kuhusiana na tukio hilo ili kupunguza taharuki katika eneo hilo.
Kwa upande wake kamanda wa jeshi la polisi mkoa wa Katavi SACP Kaster Ngonyani amethibitisha kutokea kwa tukio hilo leo majira ya saa 3 asubuhi january 21 2025 na kusema mwili wa marehemu umefanyiwa uchunguzi na madaktari na kubaini chanzo cha kifo ni kukosa hewa baada ya kujinyonga.
Hata hivyo mwili wa marehemu umehifadhiwa katika hospitali ya manispaa ya Mpanda kwa taratibu za mazishi huku jeshi la polisi likiendelea kufanya uchunguzi kubaini chanzo cha tukio hilo.