Bodaboda watakiwa kujiunga na mafunzo ya udereva
17 January 2025, 1:05 pm
“Dereva bodaboda wanapaswa kuwa na leseni ili kuondokana na migogoro na askari”
Maafisa usafirishaji maarufu kama bodaboda wametakiwa kujiunga na mafunzo ya udereva ili waweze kutambua sheria za usalama barabarani.
Hayo yamesemwa na Sajent Juliana Ibalaja kutoka kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Katavi katika kikao na madereva bodaboda kilichofanyika katika Ofisi za mtendaji wa kata ya Mpanda Hotel.
Sajent Juliana amesema kuwa madereva bodaboda wanapaswa kuwa na leseni ili kuondokana na migogoro na askari na kuwataka kutumia fursa hiyo ili waweze kupata leseni.
Kwa upande wao madereva bodaboda waliohudhuria kikao hicho wameipongeza hatua hiyo na kuahidi kujitokeza kupata mafunzo ili waweze kujua namna ya kuendesha kwa kufuata sheria za usalama barabarani.
Naye Diwani wa kata hiyo ameahidi kutekeleza mpango wa kuanzishwa kwa mafunzo hayo na kuchangia kiasi cha pesa ili kufanikisha zoezi hilo.