Zaidi ya watoto 20 huzaliwa njiti kila mwezi mkoani Katavi
22 November 2023, 10:31 am
Mama anapojihisi kuwa ni mjamzito ni bora awahi kituo cha kutolewa huduma za afya ili kuepuka kujifungua mtoto kabla ya wakati.
Na Gladness Richard-Katavi
Zaidi ya watoto 20 kila mwezi ndani ya mkoa wa Katavi wameripotiwa kuzaliwa wakiwa njiti huku chanzo kikitajwa kuwa ni kifafa cha mimba, upungufu wa damu na mtoto kuotesha kondo la chini katika uzazi.
Hayo yamesemwa na daktari kutoka katika kitengo cha watoto katika hospitali ya rufaa mkoa wa Katavi Kassimu Msuya. Ameshauri kuwa mama anapojihisi kuwa ni mjamzito ni bora awahi kituo cha kutolea huduma ya afya ili kuepuka kujifungua mtoto kabla ya wakati.
Kwa upande wao wanawake waliojifungua watoto njiti wameupongeza uongozi wa hospitali ya rufaa ya mkoa kwa kuendelea kupambana kutoa matibabu kwa watoto hao.
Siku ya Watoto Njiti Duniani huadhimishwa kila ifikapo 17 Novemba kila mwaka na mwaka huu maadhimisho hayo ambayo tayari yamefanyika yameambatana na kaulimbiu isemayo ‘Hatua kidogo, Faida kubwa, huduma ya Ngozi kwa Ngozi, kwa kila Mtoto, kila Mahali.’