MIGOGORO WAKULIMA NA WAFUGAJI HALI TETE
23 May 2022, 1:56 pm
KATAVI.
Baadhi ya wananchi wa kijiji cha Karema mkoani katavi wameiomba serikali kuchukua hatua za haraka kutatua mgogoro kati ya wakulima na wafugaji kabla haujaleta madhara makubwa katika jamii.
Wakulima hao wameiambia mpanda radio fm kuwa ugomvi kati ya wafugaji na wakulima umekuwa ukitokea mara kwa mara ndani ya kijiji hicho na kusababisha shughuli za kilimo kutofanyika ipasavyo.
Kwa upande wao baadhi ya viongozi wa kijiji hicho wameeleza namna ambavyo walivyopigwa na wafugaji wakati wakiwa katika majukumu yao ya utekelezaji wa kulinda mazao ya wananchi ambayo yanaharibiwa na mifugo.
Hali hiyo ikampelekea Mkuu wa wilaya ya tanganyika onesmo buswelu kuliagiza jeshi la polisi wilayani humo kumukamata mfugaji ajulikanae kwa jina Runyalaja Omari na wenzake wanaodaiwa kufanya fujo ikiwemo kuwapiga viongozi wa kijiji cha Karema wakati wakitekeleza majukumu yao wilayani Tanganyika.
Migogoro kati ya wafugaji na wakulima wilayani humo imekuwa ikiripotiwa mara kadhaa huku chanzo kikubwa kikitajwa kuwa ni wafugaji kuingia kulisha mifugo yao katika mashamba ya wakulima .