Wavuvi Kutaka Mali kwa Haraka Chanzo cha Uvuvi Haramu “CP Awadhi”
10 April 2023, 5:25 pm
MPANDA
Kamishna wa oparesheni na mafunzo ya Jeshi la Polisi Tanzania, CP Awadhi Juma Haji amesema moja ya changamoto zinazokwamisha mapambano dhidi ya uvuvi haramu na uhalifu kwenye maziwa ni kutokana baadhi ya wavuvi kugeukana na kutaka mali za haraka bila kufuata sheria.
CP Haji ameyasema hayo Aprili 8, 2023 katika kikao kazi cha kutathimini na kupanga mikakati ya kudhibiti vitendo vya uhalifu ziwani na uvuvi haramu katika Ziwa Tanganyika na Ziwa Rukwa, kilichofanyika mjini Mpanda kilichowakutanisha Makamanda wa Polisi kutoka Mikoa ya Kanda ya Magharibi ya Rukwa, Katavi ,Kigoma na wadau
Awali akifungua kikao hicho, mgeni rasmi ambaye pia ni Mkuu wa Mkoa wa Katavi Mwanamvua Mrindoko amewataka wadau wa sekta ya uvuvi na wananchi kwa ujumla kuwa na uzalendo kwa kutoa taarifa za viashiria vya uvunjifu wa amani na uvuvi haramu katika maziwa hayo.
RC Mrindoko amesema Serikali ya awamu ya Sita inajali na kutambua umuhimu wa sekta ya uvuvi na ndiyo maana inaendelea kufanya uwekezaji kwa kujenga mialo hivyo ameliagiza Jeshi la Polisi kuimarisha ulinzi maeneo yote ya Ziwa Rukwa na Ziwa Tanganyika ili kukomesha uhalifu na uvuvi haramu.