Joy FM
Joy FM
6 March 2026, 16:02

Mkuu wa Wilaya Kasulu Kanal Isaac Mwakisu amewataka viongozi wa serikali za mitaa kufanya kazi karibu na wananchi ili waweze kutambua changamoto zao na kuzitatua
Na Hagai Ruyagila
Watendaji wa Kata na Mitaa katika halmashauri ya Mji Kasulu Mkoani Kigoma wametakiwa kuwajibika ipasavyo, kusikiliza kero za Wananchi na kushirikiana katika utekelezaji wa majukumu yao ili kuboresha huduma kwa wananchi.
Wito huo umetolewa na Mkuu wa wilaya ya Kasulu Kanal Isaac Mwakisu wakati akizungumza na watendaji wa kata, mitaa maafisa tarafa na viongozi wa kuu wa idara wa halmashauri hiyo katika kikao cha kazi kilicholenga kuimarisha utendaji na uwajibikaji kazini.

Kanal Mwakisu amesisitiza kuwa ushirikiano na mawasiliano mazuri miongoni mwa watumishi wa umma ni muhimu katika kuhakikisha huduma bora na kwa wakati zinawafikia wananchi.
Katibu tawala wa wilaya ya Kasulu Bi. Theresia Mtewele amesema serikali imejipanga kutoa huduma bora kwa wananchi pia amewasisitiza watendaji hao kujitambua, kujenga nidhamu ya kazi na kufuata maadili na sheria za kazi huku akisisitiza mahusiano mazuri kazini.

Awali, akizungumza Afisa Mwandamizi wa TAKUKURU, Dawati la uchunguzi wilaya ya Kasulu Alfa Eliyatosha amesema mtumishi yeyote wa halmashauri hatakiwi kuikosesha halmashauri mapato kwa namna yoyote isipokuwa ni vyema kusimamia mapato yanayopatikana katika maeneo yao ya kazi ili kuinua uchumi wa halmashauri hiyo.
Afisa Mtendaji wa mtaa wa Sinza Kata ya Mwilamvya Njile Charles Akizungumza kwa niaba ya watendaji wa kata na mitaa wa halmashauri hiyo ameahidi kuendeleza ushirikiano na wafanyakazi kwa kufuata sheria, kanuni na taratibu zote za kazi ili kuchochea maendeleo ya halmashauri hiyo.