Joy FM

Wanawake waaswa kutumia fursa za kiuchumi Buhigwe

6 March 2026, 10:19

Afisa maendeleo ya jamii Mkoa Kigoma Msafiri Nzunuri akizungumza katika jukwa la wanawake Buhigwe, Picha na Tryphone Odace

Wanawake ni sehemu muhimu ya jamii na wana mchango mkubwa katika maendeleo ya familia na taifa kwa ujumla ambapo katika dunia ya sasa kuna fursa nyingi zinazowazunguka wanawake kama vile elimu, biashara, kilimo na ajira na wanapochangamkia fursa hizo wanaweza kuboresha maisha yao na ya jamii inayowazunguka.

Na Tryphone Odace

Wanawake Wilayani Buhigwe Mkoani Kigoma wameshauriwa kutumia fursa zilizopo katika Wilaya hiyo ili waweze kujikwamua kiuchumi na kusaidia kuchangia maendeleo ya familia zao na taifa kwa ujumla.

Kauli hiyo imetolewa na Afisa maendeleo ya jamii Mkoa Kigoma Msafiri Nzunuri wakati akizungumza katika jukwa la wanawake Wilayani Buhigwe lenye lengo la kujadili fursa, uwekezaji kwa wanawake pamoja na ushiriki wao katika shughuli za uzalishaji mali.

Wanawake wakiwa katika jukwa la wanawake kujadili fursa za kiuchumi Buhigwe Picha na Tryphone Odace

Amesema iwapo wanawake watachangamkia fursa mbalimbali zilizopo katika maeneo yao ikiwemo mikopo itawasaidia kuacha utegemezi kwa wenzi wao kutokana na mchango watakaokuwa wanaoutoa kwa familia na taifa kwa.

Sauti ya Afisa maendeleo ya jamii Mkoa Kigoma Msafiri Nzunuri

Kwa upande wake, Afisa ustawi wa jamii Wilaya Buhigwe amesema wanawake wana nafasi kubwa ya kuchangia katika shughuli za kiuchumi lakini wamekuwa wakishindwa kufikia azma hiyo kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo vitendo vya ukatili na kutopewa nafasi ya kuonyesha uwezo wao.

Baadhi ya wadau wa maendeleo waliohudhuria hafla ya jukwa la wanawake, Picha na Tryphone Odace
Sauti ya Afisa ustawi wa jamii Wilaya Buhigwe

Naye Afisa mradi kutoka shirika la Care International Gidion Leonard amesema kuwa vikundi kwa wanawake ni chachu ya kujiinua kiuchumi huku akisisitiza umuhimu wa wanawake kushirikiana na kuunda vikundi vitakavyowasaidia kupata mafunzo, mikopo pamoja na masoko ya bidhaa zao.

Sauti ya Afisa mradi kutoka shirika la Care International Gidion Leonard

Kwa upande wake, Katibu wa Wilaya ya Buhigwe Bi. Utefta Mahega, amewahimiza wanawake kutumia fursa zilizopo hasa mikopo inayotolewa na taasisi balimbali na kuwa Serikali inaendelea kuweka mazingira rafiki kwa wanawake kupitia mikopo ya asilimia 10 ya Halmashauri.

Katibu wa Wilaya ya Buhigwe Bi. Utefta Mahega akifungua jukwa la wanawake Buhigwe, Picha na Tryphone Odace

Jukwaa hilo limewakutanisha wanawake kutoka kata zote ishirini zinazo patikana ndani ya Wilaya ya Buhigwe na limekuwa fursa ya kujadili namna ya kuongeza ushiriki wa wanawake katika shughuli za maendeleo ya jamii.

Afisa maendeleo Wilaya ya Buhigwe Christopher Kajange akizungumza katika jukwa la wanawake, Picha na Tryphone Odace

Jukwa la wanawake Buhigwe limefanyika ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya siku ya wanawake ambapo kilele cha maadhimisho hayo kimkoa yatafanyika Wilayani Kakonko yakiwa yamebebwa na kaulimbiu isemayo “Haki kwa mwanamke na wasichana msingi wa maendeleo jumuishi kufikia dira 2050”