Joy FM

RC Kigoma aagiza soko la Kagunga lianze kutumika

11 January 2026, 15:16

Soko la kimkakati la Kagunga lililopo kata ya Kagunga Wilayani Kigoma Mkoani ujenzi wake ulianza mwaka 2009.

Mradi wa soko la kimkakati la kimataifa lililopo Kagunga lilianza kujengwa mwaka 2009 na likitarajiwa kuwanufaisha wafanyabiashara kutoka Tanzania, Burundi na hata Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo

Na Mwandishi wetu

Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Balozi Simon Sirro ameagiza kuanza kutumika kwa mojawapo ya jengo katika soko la kimkakati la Kagunga lililopo kata ya Kagunga Wilayani Kigoma Mkoani Kigoma, wakati serikali ikichukua hatua dhidi ya mkandarasi aliyetelekeza mradi huo ambao ujenzi wake ulianza mwaka 2009.

Uamuzi huo umefikiwa  mara baada ya Balozi Sirro kukagua soko hilo lililopo mpakani mwa Tanzania  na Burundi, kisha kuagiza mkandarasi anayetekeleza ujenzi wa mradi huo kukutana na kiongozi huyo ili aweze kueleza sababu za kushindwa kuendelea na kazi huku akiwa tayari amepokea kiasi cha Shilingi milioni 229 ikiwa ni malipo ya awali.

Mkuu wa Mkoa Kigoma akipokea taarifa ya mradi wa soko la Kagunga, Picha na Ofisi ya mawasiliano Kigoma

Amesema serikali ya mkoa haitoweza kumvumilia mkandarasi atakayeshindwa kutekeleza majukumu yake na kukwamisha kasi ya utoaji wa huduma kwa wananchi.

Mkuu wa Mkoa Kigoma akiwa amewasili katika soko la Kagunga, Picha na Ofisi ya mawasiliano Kigoma

Akitoa taarifa ya mradi, Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Kigoma Exavery Ntambala amesema mradi huo uliibuliwa na wananchi wenyewe ili kuimarisha biashara kati ya Tanzania, Burundi na Jamhuri ya Kidemoktasia ya Congo.

Amesema mradi umekuwa ukitelekezwa na wakandarasi mbalimbali kwa nyakati tofauti huku mkandarasi aliyepo naye akishindwa kuuendeleza huku akiwa amekwisha kupokea malipo ya awali.

Muonekano wa jengo la soko ambalo halijakamilika ujenzi ukiendelea, Picha na Ofisi ya mawasikiano Kigoma