Joy FM
Joy FM
17 September 2025, 09:37

Mtoto aliyetelekezwa na mama yake akiwa darasa la pili na kulelewa na shule ahitimu masomo ya darasa la saba huku wito ukitolewa kwa wadau kujitokeza kumsaidia.
Na Hagai Ruyagila
Wazazi na walezi wilayani Kasulu mkoani Kigoma wametakiwa kuacha tabia ya kuwatelekeza watoto wao pindi wanapokumbwa na changamotoya za kifedha, hususan kushindwa kulipa ada katika shule binafsi hali ambayo inaathiri maendeleo ya watoto kielimu na kisaikolojia.
Wito huo umetolewa na Mkurugenzi wa shule ya Gahima Mwl, Nkonko Eliud wakati wa mahafali ya darasa la saba yaliyofanyika katika shule hiyo iliyopo Mjini Kasulu.
Amesema baadhi ya wazazi wamekuwa wakitelekeza watoto wao shuleni kwa kushindwa kulipa ada bila kutoa taarifa wala kuweka mawasiliano jambo ambalo ni ukiukwaji wa haki za msingi za mtoto.
Mwl, Nkonko ametoa mfano wa tukio la kusikitisha kwa mwanafunzi Mmoja ambaye amehitimu darasa la saba shuleni hapo kutelekezwa na mama yake tangu akiwa darasa la pili na kutoweka bila kuacha taarifa yoyote.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Jumuiya ya wazazi wilaya ya Kasulu na mgeni rasmi katika mahafali hayo Bw, Seleman Malumbo amesikitishwa na kitendo hicho licha ya kumpongeza mkurugenzi huyo kwa moyo wake wa huruma kuhakikisha mtoto huyo anamaliza masomo yake ya msingi.

Mwenyekiti wa bodi ya shule hiyo Ruth Mwegerano amewatia moyo wahitimu kwa kuwataka kuzingatia masomo kwa bidii na kutokata tamaa licha ya changamoto zinazowakumba.
Katika hatua ya kuonyesha mshikamano na kuguswa na changamoto ya mwanafunzi huyo aliyetelekezwa na mzazi wake, Wazazi na wageni waliokuwepo kwenye mahafali hayo wamemchangia kiasi cha shilingi 701,300/=
Pia mdau wa elimu Leonard Magaba amejitolea kugharamia masomo ya mwanafunzi huyo katika ngazi ya sekondari na kuahidi kumpatia mahitaji muhimu.
