Joy FM
Joy FM
25 July 2025, 12:42

Halmashauri ya Mji wa Kasulu mkoani Kigoma inakabiliwa na upungufu wa lita milioni 5 za maji kati ya lita milioni 15 zinazohitajika ili kuondoa changamoto ya uhaba wa maji safi na salama kwa wananchi.
Na Hagai Ruyagila
Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso amemuagiza mkandarasi wa Mradi wa Maji wa Miji 28 uliopo halmashauri ya Mji wa Kasulu mkoani Kigoma kuhakikisha anakamilisha kazi hiyo kwa wakati.
Katika ziara hiyo Mhe Aweso ametoa maagizo hayo baada ya kutembelea na kukagua maendeleo ya mradi huo ambapo amesema kuwa serikali haitavumilia ucheleweshaji wowote wa utekelezaji wa mradi huo muhimu kwa wananchi huku akimtaka mkandarasi kuongeza kasi na ufanisi maana fedha zipo.

Mkuu wa Wilaya ya Kasulu, Kanali Isaac Mwakisu, amezungumzia upatikanaji wa huduma ya maji katika wilaya ya Kasulu na namna serikali inavyoendelea kupambana kutatua changamoto ya huduma ya maji katika wilaya hiyo.
Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira wilayani Kasulu, Mhandisi Hussein Nyemba, ameelezea hatua ya mradi huo ulipofikia na namna utakavyokwenda kuwa msada kwa jamii katika halmashauri ya mji wa Kasulu.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Kasulu, Mbelwa Chidebwe, ameipongeza serikali kwa juhudi za kupeleka maendeleo kwa wananchi kupitia miradi ya kimkakati kama huo wa maji, akisisitiza kuwa chama hicho kitaendelea kushirikiana na serikali kusukuma mbele maendeleo ya wananchi.
Wananchi wa Halmashauri ya Mji wa Kasulu wamesema wanatumaini kuwa mradi huo utakapokamilika, utasaidia kwa kiasi kikubwa kuboresha hali ya upatikanaji wa maji na kuinua maisha ya wakazi wa mji huo.
