Joy FM
Joy FM
15 July 2025, 13:20

Wakati zikiwa zimesalia siku chache kabla ya uchaguzi Mkuu wa mwezi oktoba viongozi na wafuasi wa vyama vya siasa wametakiwa kutenda haki
Na Hagai Ruyagila
Wajumbe wa vyama vya siasa mkoani Kigoma wanaoshiriki katika mchakato wa kura za maoni kwa ajili ya kuwapata wagombea wa nafasi za uongozi nchini wametakiwa kutenda haki na kuzingatia misingi ya demokrasia ndani ya vyama vya siasa, bila upendeleo au kushinikizwa na mtu yeyote.
Wito huo umetolewa na Askofu wa Kanisa la Anglikana, Dayosisi ya Western Tanganyika Mhashamu Emmanuel Bwatta wakati akizungumza na waumini wa kanisa hilo.
Amesisitiza kuwa ni wajibu wa kila mjumbe kuhakikisha anatoa uamuzi wa haki katika kura za maoni ili kuwapata wagombea bora watakaoliwakilisha vema taifa katika uchaguzi mkuu ujao.
Aidha Askofu Bwatta ametoa onyo kwa waumini wa kanisa hilo kujiepusha na vurugu hasa vijana na kutii sheria za nchi zilizowekwa.
Baadhi ya wajumbe kutoka katika vyama mbali mbali vya siasa akiwemo Vedasco Kagina kupitia chama cha wananchi CUF na Samola Bodi kupitia CCM wamesema wako tayari kutenda haki na kufuata sheria na taratibu zilizopo ndani ya vyama vyao.
Mchakato wa kura za maoni kwa vyama mbali mbali vya siasa nchi Tanzania unaendelea kuelekea uchaguzi mkuu, ambapo vyama vinapitia hatua za ndani kuwachagua wagombea watakaowania nafasi ya Udiwani, Ubunge na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.