Joy FM

BoT yatoa elimu ya usalama katika fedha kwa watu wenye uoni hafifu

22 May 2025, 16:57

Ni watu wenye mahitaji maalum hasa uoni hafifu wakiwa katika mafunzo ya utambuzi wa alama za usalama katika fedha na majukumu ya Benki Kuu Tanzania (BoT)

Watu wenye mahiataji maalum wakiwemo wenye uoni hafifu wilayani Chamwino mkoani Dodoma wametakiwa kufuatilia na kutambua alama za usalama katika fedha pamoja na utunzaji unaofaa wa fedha.

Na Glory Paschal

Benki Kuu ya Tanzania BoT imetoa elimu ya fedha kwa kundi la watu wenye mahitaji maalum ili waweze kutambua alama za usalama katika fedha wakati wa matumizi katika shughuli zao.

Akizungumza wakati wa mafunzo hayo, Afisa wa Benki Kuu ya Tanzania BoT, Atifigwege Mwakabalula amesema wameamua kutoa elimu hiyo ili kulisaidia kundi la watu wenye mahitaji maalum yaani uoni hafifu ili waweze kutumia noti za fedha na kuzingatia utunzaji unaofaa.

Afisa wa Benki Kuu ya Tanzania BoT, Atifigwege Mwakabalula akiwa anatoa elimukwa watu wenye mahitaji maalumu

Katika mafunzo hayo yaliyofanyika wilayani Chamwino mkoani Dodoma  Bw. Atifigwege Mwakabalula amesema watu wenye ulemavu au uoni hafifu wamekuwa wakikabiliwa na changamoto za utambuzi wa noti salama kwa kutokuona alama za usalama pamoja na elimu ya fedha.

Aidha katika mafunzo hayo ameeleza majukumu ya Benki Kuu ya Tanzania BoT huku akiwataka kundi hilo linalojulikana kama Tanzania League of Blindness TLB kuendelea kuweka na kutunza fedha katika mazingira salama.