Joy FM

Serikali kuendelea kudhibiti uhalifu wa kifedha

15 April 2025, 11:25

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akisalimiana na Gavana wa Benki kuu BoT Emmanuel Tutuba akiwasili katika mkutano kati ya ujume wa Tanzania na kikosi cha kimataifa, Picha na BoT

Serikali kuendelea kusimamia na kudhibiti uhalifu wa kifedha

Na Glory Enock Paschal

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema kuwa Tanzania itaendelea kushiriki na kutimiza matakwa ya kimataifa katika kupambana na kudhibiti uhalifu wa kifedha.

Amesema kuwa Tanzania inatambua changamato za uhalifu wa kifedha na imejidhatiti katika kudhibiti hali hiyo kwa viwango vya kimataifa vilivyopo.

Amesema hayo leo Jumatatu (Aprili 14, 2025) wakati Ufunguzi wa Mkutano kati ya Ujumbe wa Tanzania na Kikosi Kazi cha Kimataifa cha Kudhibiti Fedha Haramu, kwenye ukumbi wa Benki Kuu ya Tanzania jijini Dar es Salaam.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akizungumza wakati Ufunguzi wa Mkutano kati ya Ujumbe wa Tanzania na Kikosi Kazi cha Kimataifa cha Kudhibiti Fedha Haramu, Picha na BoT

Amesema kuwa kufuatia tathmini zilizofanywa na taasisi za Kuthibiti Uhalifu wa Kifedha Kusini Mashariki mwa Afrika mwaka 2021 na Kikosi cha Kimataifa cha Ushirikiano na Tathmini ya mwaka 2022, Tanzania imeimarisha mifumo ya kupambana na fedha haramu ikiwemo kujengea uwezo wa rasilimali watu na vifaa taasisi zinazohusika katika mapambano hayo.

Waziri Mkuu ameyataja maeneo yaliyofanyiwa kazi kuwa ni mabadiliko ya sheria na sera, matumizi ya takwimu na teknolojia, kuimarisha sekta nyumba na ardhi, kuwajengea uwezo wadau na kuimarisha usimamizi wa Taasisi za za kifedha.

Kwa upande wake, Waziri wa Fedha Dkt. Mwigulu Nchemba amesema kuwa Tanzania baada ya kupokea mpango kazi kutoka Kikosi Kazi cha Kimataifa cha Kupambana na Fedha Haramu ilifanya maamuzi ya ngazi ya juu ya kuimarisha usimamizi uhalifu wa kifedha nchini hali ambayo imeonesha mafanikio makubwa.

Washiriki wa Mkutano kati ya Ujumbe wa Tanzania na Kikosi Kazi cha Kimataifa cha Kudhibiti Fedha Haramu, Picha na BoT