Joy FM
Joy FM
9 April 2025, 13:20

Mkuu wa Wilaya ya Kasulu Kanali Isaac Mwakisu amewaomba wananchi kutozuia ujenzi wa mradi kwani serikali itahakikisha wanalipwa fidia zao
Na Hagai Ruyagila
Serikali katika halmashauri ya mji Kasulu Mkoani Kigoma imejipanga kumaliza mgogoro wa Ardhi katika kata ya Nyumbigwa kufuatia wananchi kugomea mradi wa ujenzi wa maji taka katika kata hiyo.
Katika mkutano wa wananchi na kamati ya Ulinzi na usalama wilaya ya Kasulu uliofanyikia katika kata ya Nyumbigwa, Baadhi ya wananchi wameomba kulipwa fidia kwenye maeneo yao ambayo utekelezaji wa mradi wa maji taka unaotarajiwa kutekelezwa katika kata hiyo huku wakiomba ushirikishwaji kabla ya mradi kuanza kutekelezwa ili kuepuka migogoro ya ardhi.

Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Nyumbigwa Benjamini Chalukura ameiomba serikali kufuata utaratibu ili kuwasaidia wananchi ambao mradi huo utapita katika maeneo yao.
Afisa Ardhi halmashauri ya Mji Kasulu Pesha Jackson anasemaje kuhusu eneo hilo?
Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya Mji Kasulu Mwl, Vumilia Simbeye amesema suala hilo litatafutiwa ufumbuzi kwakuwa dhamira yao ni kuijenga jamii yenye amani na upendo.

Mkuu wa wilaya ya Kasulu Kanali Isaac Mwakisu amewaomba wananchi kutozuia ujenzi wa mradi huo wakati utaratibu wa kuangalia uhalali wa maeneo ya wananchi kulipwa fidia ukiendelea kufanyiwa kazi.