Joy FM
Joy FM
7 March 2025, 09:43

Jamii mkoani Kigoma imeaswa kuwa na desturi ya kupanda miti ili kusaidia kuendelea kutunza mazingira na kupunguza mabadiliko ya tabianchi.
Na Timotheo Leonad
Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira NEMC Kanda ya Magharibi, imegawa miti zaidi ya elfu moja kwa shule tano za wilaya ya Kigoma lengo likiwa ni kuhamasisha utunzaji wa mazingira.

Kauli hiyo imetolewa na Edith William Makungu ambaye ni Afisa Mwandamizi kutoka NEMC Kanda ya Magharibi wakati wa ugawaji wa miti kwa shule mbalimbali ikiwa ni sehemu ya mwendelezo wa maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani.
Amesema malengo ya kugawa miti kwa shule hizo ni kuwawezesha watoto wakiwa bado wadogo kufahamu umuhimu wa upandaji wa miti na utunzaji wa mazingira kwa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Kwa upande wake Mkuu wa Shule ya Alpha Adventist Pre and Primary school Mwalimu James Chirstopher ameahidi kuitunza miche hiyo huku akiipongeza serikali kwa kuwapatia miti hiyo.
Baadhi ya wanafunzi waliokabidhiwa majukumu ya kuitunza miti hiyo wameipongeza NEMC na kuahidi kuitunza miti hiyo ili kutunza mazingira na kuhakikisha inasaidia kupata hewa safi wakiwa mazingira ya shuleni.
