

26 February 2025, 14:38
Serikali imeendelea kuboresha elimu nchini kwa kujenga vyumba vya madarasa ili wananfunzi waweze kupata elimu bora.
Na Hagai Ruyagila
Mamlaka ya Elimu Tanzania TEA imekabidhi mradi wa nyumba nne kwa shule ya sekondari Nyumbigwa na madarasa matatu katika shule ya Msingi Msivyi halmashauri ya Mji Kasulu mkoani Kigoma yenye thamani ya shilingi milioni 160 ili kurahisisha mfumo wa utoaji elimu kwa wanafunzi na waalimu kuwa rahisi kwenye ufundishaji na ujifunzaji.
Hayo yamebainishwa na Mwakilishi wa Mkurugenzi mkuu wa taasisi ya mamalaka ya elimu Tanzania (TEA) Paulo Kawawa ambaye ni afisa elimu miradi wa mamlaka ya elimu Tanzania amesema miradi hiyo imejengwa kuanzia mwaka wa fedha 2020 / 2021, 2021 / 2022, 2022 / 2023 na 2023 /2024 na lengo la serikali ni kutoa msaada unaoenda kurahisisha utoaji wa elimu katika suala la ufundishaji na ujifunzaji.
Kwa upande wake Mwalimu mkuu wa shule ya msingi Msivyi Metusela Maliatabu amesema kukamilika kwa ujenzi wa madarasa hayo umesaidia kuongeza ufaulu na kupunguza utoro kwa wanafunzi wa shule hiyo japo bado kuna changamoto zinazo endelea kuikabili shule hiyo ikiwemo uhaba wa madarasa na nyumba za waalimu.
Diwani wa kata ya Muganza Ezron Budulege ameishukuru serikali kwa namna ilivyosaidia shule hiyo kupata madarasa matatu ambayo yatapunguza changamoto ya miundombinu shuleni hapo.
Nao baadhi ya wanafunzi wa shule ya msingi Msivyi wamezungumzia namna bora ambayo serikali imepunguza changamoto katika shule hiyo katika suala zima la ujifunzaji shuleni hapo.