Joy FM

Mkataba ujenzi visima sita vya umwagiliaji wasainiwa Kigoma

12 February 2025, 09:17

Baadhi ya wataalam wa kilimo baada ya kutia saini mkataba wa uchimbaji visima kilimo cha umwagiliaji, Picha na KGPC

Serikali imesema itaendelea kuhakikisha inaimarisha sekta ya kilimo kwa kuweka miundombinu rafiki kwa wakulima ili kuhakikisha wanalima kilimo chenye tija.

Na James Jovin

Wakazi mkoani Kigoma wameishukuru serikali kwa kuendelea kuwekeza katika miradi ya ujenzi wa miundombinu wezeshi kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji hali inayochangia kuboresha uchumi wao kupitia sekta ya kilimo.

Shukurani hizo zimetolewa kufuatia serikali kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji kusaini mkataba na Mkandarasi Waterweys Hydrotech Ltd kwa ajili ya kutekeleza mradi wa uchimbaji na ujenzi wa visima sita (6) vya umwagiliaji kwa thamani ya zaidi ya Shilingi Mil. 200  katika wilaya  za Kasulu, Uvinza, Kibondo na Kakonko.

“Tunatarajia kuondokana na adha ya Kilimo cha msimu, kupata mazao hafifu na kinyume na matarajio, migogoro ya kugombania maji huku tukitarajia kuinua pato letu kupitia Kilimo” amesema Rhoda Samwel mkazi wa kijiji cha Rusesa wilayani Kasulu.

Zoezi la utiaji saini Mkataba wa uchimbaji visima vya kilimo cha umwagiliaji, Picha na KGPC

Akimwakilisha Mkurugenzi wa Tume ya Umwagiliaji nchini kwenye hafla ya utiaji saini mkataba huo iliyofanyika katika kijiji cha Rusesa wilayani Kasulu Mkoani hapa, Mha. Katuta Mustang ambaye ni Mhandisi Umwagiliaji Mkoa wa Kigoma amesema serikali imedhamiria kuhakikisha wananchi wanalima kilimo chenye tija na kujihakikishia utoshelevu wa mazao ya chakula na biashara.

Aidha Mha. Katuta amesema mradi huo unaotekelezwa chini ya Programu ya mifumo himilivu ya chakula kwa kuzingatia matokeo, utakamilika katika kipindi cha miezi mitatu kuanzia februari 26, 2025 na utawanufaisha zaidi ya wakulima 500 katika vijiji vya Ruyenzi (Kakonko), Kasangezi na Rusesa (Kasulu), Ruchugi (Uvinza), Munyegera (Buhigwe), Kumbanga na Kalalangona(Kibondo).

Akizungumza kabla ya kushuhudia utiaji saini wa mkataba huo, Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Mh. Thobiasi Andengenye ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa kuendelea kuigusa Sekta ya Kilimo kwani kuimarika kwake kutaimarisha uwezo wa kujimudu kiuchumi kwa wananchi na Taifa kwa ujumla.

Mkuu wa Mkoa Kigoma akisalimia wananwanchi wa reusesa wakati wa utiaji saini mkataba wa umwagiliaji, Picha na KGPC

Ameendelea kusisitiza kuwa kupitia usimamizi wa serikali, Wizara ya Kilimo imefanya mapinduzi makubwa kwa uchumi wa Taifa jambo linaloongeza tija kiuzalishaji na kukifanya kilimo kuwa katika mfumo wa kibiashara zaidi.